IDARA YA FEDHA
KITEGO CHA MAPATO
Idara ya Fedha ni uti wa mgongo wa Halmashauri kwa sababu ya umuhimu wake katika kukusanya, kusimamia, kupanga matumizi ya Fedha za Halmashauri katika Idara mbalimbali. Kupitia Idara hii ndipo ambapo Idara zingine huwezeshwa kukamilisha shughuli za utoaji wa huduma bora utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pamoja na Sehemu nyingine zinazounda Idara hii tutajikita zaidi kuelezea kuhusu Sehemu ya Mapato kutokana na umuhimu wake katika upatikanaji wa fedha katika Halmashauri. Majukumu ya Sehemu hii ni:
•Kusimamia na kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo vya Halmashauri
•Kubuni vyanzo vipya vya mapato
•Kuandaa na kuboresha kanzidata ya vyanzo vyote vya mapato
•Kutunza kumbukumbu za walipa Kodi
VYANZO VIKUU VYA MAPATO YA NDANI
•Kodi ya Majengo
•Kodi ya huduma
•Leseni za Biashara
•Ushuru wa mabango
•Ushuru wa maegesho ya Magari
•Kodi ya Pango
•Ushuru wa Stendi za Mabasi
•Ushuru wa Masoko
Vyanzo hivi vya mapato vinachangia 87% ya mapato yote ya ndani, vinavyobaki huchangia 13% tu.
1.KODI YA MAJENGO (PROPERTY TAX)
Kodi ya Majengo ni kodi inayotozwa kwenye Majengo yote yaliyopo kwenye eneo la Utawala la Jiji la Arusha. Wamiliki wa majengo haya hupaswa kulipa kodi hii kila mwaka kulingana na thamani ya Jengo analomiliki. Kodi hii iko kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Majengo Na. 2 ya mwaka 1983 (Urban Authority Rating Act, No. 2, 1983)
•VIWANGO VYA KODI YA MAJENGO
i.Uthamini wa Majengo (Property Valuation) – Uthamini wa majengo hufanywa na halmashauri ya Jiji na mmiliki atapewa hati ya madai kulingana na thamani ya Jengo lake. Uthamini wa majengo hutofautiana kati ya jengo moja na lingine kulingana na kiasi cha uwekezaji kilichofanyika na eneo ambapo Jengo hilo linapatikana.
ii.Viwango Mlingano (Flat Rate System) – Viwango hivi hutozwa kwa mujibu wa Sheria ndogo ya Halmashauri inavyoelekeza namna ya kutoza Kodi ya Jengo katika maeneo ambayo hayajafanyiwa uthamini. Hii hutozwa kwa kiwango sawa katika eneo lililoainishwa.
•MUDA WA KULIPA KODI YA JENGO
Kodi ya Jengo hulipwa bila tozo kuanzia tarehe 01 Januari mpaka tarehe 31 Machi ya kila mwaka, baada ya Aprili mosi tozo la riba ya asilimia moja (1%) hutozwa kwa kila mwezi utakaochelewa. Ukilimbilikiza kodi ya Jengo kwa zaidi ya mwaka mmoja utatozwa faini ya asilimia hamsini (50%) kama adhabu.
•MAJENGO YANAYOTOZWA (PROPERTY CHARGED)
Majengo yanayotozwa ni yale yaliyojengwa kwa vifaa vya kudumu kama vile matofali ya aina yeyote, vyuma mbalimbali. Nyumba za udongo hazitozwi kodi ya Jengo.
•MAJENGO YENYE MSAMAHA WA KODI (PROPERTY TAX EXEMPTION)
Kwa mujibu wa Sheria Kodi ya Majengo husamehewa kwa majengo yote yanayotumiwa na Serikali, Nyumba za kuabudia, Nyuma za kuishi wazee waliostaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria na endapo mzee huyu atapangisha nyumba hiyo atatozwa Kodi hii na pia endapo Jengo lolote kati ya haya litabadilishwa umiliki ama matumizi litatozwa pia.
2.USHURU WA HUDUMA (SERVICE LEVY)
Ushuru wa huduma ni kodi inayotozwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa no. 9 ya mwaka 1982 na sheria ndogo za Halmahauri ya Manispaa ya Arusha ya mwaka 2003. Kila mmiliki wa Kampuni ama Taasisi binafsi inayofanya shughuli zake katika mamlaka ya Halmashauri ya Jiji la Arusha kila mwaka wa Fedha anapaswa kulipa ushuru wa Huduma kwa Halmashauri ambao ni sawa na asilimia 0.3% ya mapato yake baada ya kuondoa kodi ya ongezeko la thamani na Kodi ya Mlaji kutoakna na shughuli zote alizozifanya ndani ya mipaka ya Jiji.
•GHARAMA ZA USHURU WA HUDUMA
Kila mmiliki wa Kampuni au Taasisi binafsi atapewa fomu maalumu (Service Levy Declaration Form) kwa ajili ya kuonyesha mauzo ghafi (Gross Turn Over). Mmiliki wa kampuni atatakiwa kujaza Fomu hii kwa usahihi na kuiwasilishwa kwenye Ofisi ya Mapato iliyopo katika Halmashauri ya Jiji ili kukokotolewa na kufamishwa kiasi anachotakiwa kulipa.
•MUDA WA KULIPA USHURU WA HUDUMA
Kodi hii hulipwa kila mwezi na endapo itacheleweshwa katika kipindi husika utatozwa riba ya 30% (Compoud surcharge of 30% per month). Kushidwa kuwasilisha malipo haya kwa mwaka husika utatozwa faini ya 50% ya kiasi ambacho hakikuwasilishwa.
3.KODI YA MABANGO
Kodi y Mabango ni kodi inayotozwa kwenye mabango yote yaliyopo kwenye eneo la Utawala la Jiji la Arusha. Kodi hii hutozwa kwa mujibu wa sheria No. 242/2009 na Sheria Ndogo ya Halmashauri ya Manispaa ya Arusha No. 4 Kifungu 11 na 12 No. 226/2008).
•GHARAMA ZA KODI YA BANGO
Mabango yanayowaka (Illuminated) ni Tsh 120,000 kwa kila square mita moja kwa mwaka na mabango yasiyowaka (Non Illuminated) ni Tsh 80,000 kwa kila square mita moja kwa mwaka, Maandishi ya ukutani (Waal sign roof painted & Advertisement) Tsh 15,000 kwa kila square mita kwa mwaka. Mabango yote ya vitambaa, burners, posters, Tear Drop, Roll up burner zinazowekwa barabarani au kwenye round about (Keep left) zitazlipiwa Tsh 15,000 kwa kila moja mara idadi ya siku zitakazowekwa katika eneo hilo.
4.LESENI ZA BIASHARA
Ni utaratibu wa kurasimisha uhalali wa biashara yako iweze kutambulika na mamlaka husika nchini. Leseni hii hutolewa chini ya Sheria ya Biashara Na. 25 ya mwaka 1972 na marekebisho yake yaliyofanyika mwaka 1980.
•UPATIKANJI WA LESENI ZA BIASHARA
i.Mfanyabiashara anapaswa awe na hati ya usajili iwapo anatumia jina la biashara (Certificate of Registration or Incorporation)
ii.Kama ni Kampuni mwombaji awe na “Memorandum of Article of Association” ambazo zinaonyesha kuwa kampuni imeruhusiwa kufanya biashara anayoiomba.
iii.Awe na mahali/ Eneo linalokubalika kwa aina ya biashara anayoiomba naisiwe vibanda vilivyopo kando kando ya barabara.
iv.Mfanyabishara aje na kivuli cha Cheti cha namba ya mlipa kodi (TIN) pamoja na kivuli cha cheti kinachoonyesha kuwa umelipa mapato kwa mujibu wa Sheria (Tax Clearance) ambavyo vyote vinatolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
v.Masharti mengine ya kupata Leseni hutegemea aina ya biashara mtu anayotaka kuanzisha eg. Mgahawa inadidi afuate taratibu zote za afya na kupima wafanyakazi wake.
vi.Hati ya Utaalamu (Professional Certifucates) kwa biashara zote za kitaalam.
.
AINA ZA LESENI
i.Leseni za vileo
Biashara ya vileo inatekelezwa kwa kufuata Sheria ya mwaka 1968, Kifungu 28 (Liquor License Act No. 28 of 1968) na marekebisho ya sheria hiyo yaliyofanywa mwaka 2004
•Upatikanaji wa Leseni za Vileo
Maombi yote mapya ya Leseni za vileo ni lazima yapitishwe na wataalam ambao wameainishwa kwenye Fomu ya maombi (Afisa Biashara, Ardhi, Afisa Biashara, Polisi na Mwenyekiti wa Kamati ya maendeleo ya Kata husika. Maombi yote yanayorudiwa (Renewal) yawasilishwe moja kwa moja kwa Afisa biashara anayeshughulikia leseni za vileo kwa utekelezaji.
Leseni za vileo hutolewa kwa vipindi viwili (2) ambapo kipindi cha kwanza huanzia tarehe 1/04 hadi 30/09 na kipindi cha pili huanzia tarehe 1/10 hadi 31/03 mwaka unaofuata.
ADA:
Maombi mapya na yanayorudiwa hulipiwa ada ya Jumla ya Tsh. 40,000 – kwa wale wanaouza pombe katika maeneo yao ya biashara (Retailers On) na ada ya fomu Tsh 2,000/= na kwa wale wanaouza Pombe za Kienyeji hulipia ada ya Tsh. 12,000/=
.
Aidha wanaoendesha biashara ya vileo bila kufuata taratibu zilizotajwa hapo juu huchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa Mahakamani kulipishwa faini pamoja na penalty au kufungiwa biashara zao.
ii.Leseni za biashara mbalimbali
Lesseni hii inatolewa chini ya sheria namba 25 ya mwaka 1972 na marekebisho yake ya mwaka 1980. Kila mfanyabiashara halali anapaswa kulipia leseni ya biashara husika na gharama hutofautiana kati ya biashara moja na nyingine.
Adhabu:
Mfanyabiashara atakayekutwa anafanya biashara bila kuwa na Leseni atatozwa faini ya kuanzia TSh. 50,000 - Tsh.300, 000/ = au kupelekwa mahakamani hii imeainishwa kutoka kifungu Na. 10 (1) (b). Kiwango cha faini ya kuchelewa kulipa leseni kitategemea muda uliopita baada ya leseni ya awali kuisha muda wake.
5.USHURU WA MAEGESHO
Ushuru wa maegesho unatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za mitaa na sheria ndogo za halmashauri. Magari yataegeshwa kwenye mitaa yote ya katikati ya Jiji (Central business District) iliyoainishwa kwa kuchorwa mistari inayoonyesha eneo maalumu la kuegesha. Kutakua na ada itakayolipwa kwa kila gari litakaloegeshwa katika sehemu ya kuegeshea magari, na inaweza kulipwa aidha kwa saa, kwa siku au kwa mwezi. Iwapo mtu atalipa ada ya Uegeshaji kwa siku au kwa mwezi ataruhusiwa kuegesha Gari lake katika mtaa wowote ule kwa muda aliolipia bila ya kudaiwa tena.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa