Halmashauri ya Jiji la Arusha mapema hapo jana limefanikiwa kuketi kikao cha robo ya nne kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo Madiwani, Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha na wananchi waliohudhuria kikao hicho walipata fursa ya kumkaribisha Mkurugenzi mpya wa Jiji la Arusha Dr. Maulid Suleiman Madeni.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha pia kiliambatana na zoezi la kumchagua Naibu Meya wa Jiji zoezi ambalo hufanyika katika kila robo ya nne ya kikao cha baraza la madiwani ambapo Mhe. Paul Mattysen, Diwani wa kata ya Moshono alifanikiwa kupita katika uchaguzi huo.
Sambamba na hayo Mwenyekiti wa baraza ambaye ni Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha aliendesha zoezi la uchaguzi wa wenyeviti mbalimbali wa kamati za kudumu za Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwemo Fedha na Utawala, Elimu, Maadili na Uchumi kwa mwaka huu mpya wa Fedha wa 2018/2019.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha alipokuwa akitoa neno la shukrani alisema kuwa, ushirikiano baina ya Viongozi, Madiwani na Watumishi ndio msingi wa kusogeza mbele gurudumu la maendeleo kwa wananchi wa Jiji hili.
“Katika nchi hii hakuna mwenye kibali cha kubaki kwenye madaraka milele hivyo kila mmoja kwenye nafasi yake anapaswa kuwajibika ipasavyo kwaajili ya jamii yake” aliongeza Dr. Madeni
Naye Mstahiki Meya Mhe. Kalist Lazaro alimpongeza Mkurugenzi huyo kwa kuteuliwa na kuahidi kumpatia ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu ya Halmashauri kwa maslahi ya wana Arusha na Taifa kwa ujumla.
Aidha kikao hicho cha baraza la Madiwani kiliweza kupokea taarifa mbalimbali kutoka katika taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zinazotoa huduma kwa wananchi wa Jiji la Arusha ikiwemo taarifa ya utekelezaji wa wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) kwa mwaka wa fedha 2017/2018 iliyowasilishwa na Ndg. Fodia Mwankenja, Meneja wa TARURA Jiji la Arusha .
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa