Shirika la CWCD (Centre for Women, Children and Youth Development) kwa ufadhili wa CRVPF kushirikiana na asasi zingine zisizo za kiserikali ambazo ni FAE, TCYLO, AVUREFA, wamefanya kikao cha utambulisho wa kupanga na kujifunza vitendo vya ukatili kwa watoto na vijana rika kwa timu ya Wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa lengo la kubaini, kukabiliana na kuzuia vitendo hivyo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Mkurugenzi wa mradi huo Bi. Hindu Ally Mbwego amesema kutokana na hali ilivyo kwa sasa Shirika hilo limekuwa likifanya juhudi za kuzuia ukatili dhidi ya watoto badala ya kuchukua hatua baada ya ukatili kutokea na kuongeza kuwa kwa kushirikiana na mashirika mengine pamoja na wataalam wa Halmashauri kutachagiza kufikisha ujumbe na kuifikia kundi kubwa la watu katika Jamii kwa haraka na ufanisi zaidi.
Naye Mratibu wa Miradi kutoka Shirika la Today's Children and Youth Life Organization Bw. Andrew Buhuba amesema lengo la mpango huo ni kuondoa kabisa mizizi ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na vijana wa awali, huku jitihada zaidi ikiwa kuyazuia matukio hayo kwa kuanzia kwenye vyanzo visababishi kabla ukatili haujawafikia.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dk. Kheri Kagya kwa upande wake ameishukuru CWCD na wadau kwa kuja na mpango huo na kuwasisitiza kutilia mkazo kwani vitendo hivyo vipo na kwamba wao kama wataalam wapo tayari kushirikiana nao kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kikamilifu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Bw. Onesmo Mandike amesema kama Jiji wanasifu hatua za mpango huo na kuupokea kwa kuwa una tija kwa nyakati hizi na kutoa rai kwa wadau hao kuchukulia suala hilo kwa uzito unaotakiwa na kujua kuwa hayo ni kwa manufaa ya taifa letu kwa ujumla.
Aidha Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maxmillian Iranqhe wakati akifungua kikao hicho amewahakikishia wadau hao kuwa Jiji linaunga mkono jitihada wanazofanya na kuwataka mpango huo uwe endelevu katika Kata zote za Halmashauri ili kuokoa na kustawisha kizazi kijacho kwani watoto na vijana wa awali ni Taifa la Kesho.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa