Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ameagiza wataalamu wa Afya wanapofanya uchunguzi kwa watoto waaangalie pia kama wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji.
Amesema hayo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika jana jijini hapa na kuongeza kuwa baada ya Ngariba kuzuiwa kufanya ukeketaji kwa vijana wa kike sasa wamebadilisha mbinu zao na kuanza kukeketa vichanga.
Amesema matukio ya ukatili wa jinsia ni mengi kuliko matukio ya ujambazi hapa nchini ndio maana Serikali imeanzisha madawati 500 ya Jinsia kwa Jeshi la polisi kote nchini pamoja na kuanzisha namba mpya ya simu Na. 116 ambapo mtu yoyote ambaye amefanyiwa ukatili wa kijinsia anaweza kuitumia kupata msaada.
Ameongeza kuwa Serikali pia imeanzisha madawati ya kamati ya ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto katika ngazi ya Mkoa hadi Wilaya kwa lengo la kuhakikisha haki zote za Msingi kwa watoto zinalindwa na kutekelezeka ili watoto watanzania waweze kushiriki kikamilifu katika Tanzania ya viwanda.
Pia Naibu Waziri huyo ametumia sehemu ya maadhimisho haya kuzindua kamati ya ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto mkoani Arusha na kuwakabidhi Mwongozo uliondaliwa na Wizara kama nyenzo ya kufanyia kazi kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Wakati huo huo Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Bi. Sihaba Nkinga katika hotuba yake kumkaribisha Mgeni rasmi amesema maadhimisho ya mtoto wa Afrika yanatoa nafasi kwetu sisi watanzania kutafakari na kujitathimini ni namna gani tunatekeleza kwa vitendo haki za Msingi za watoto.
Bi. Sihaba amesema kuwa Maadhimisho haya kimsingi yanaadhimishwa Kitaifa kila baada ya miaka mitano lakini pia huadhimishwa kila mwaka katika ngazi ya Mkoa na Wizara kwa kuzingatia agenda iliyopo hivyo Arusha inaongoza kwa mikoa mitano yenye ukatili mkubwa kwenye eneo la ukeketaji.
Amezitaja haki za watoto kuwa ni haki ya kusikilizwa, kuendelezwa, kuishi, kulindwa na kutobaguliwa lakini pia amesema kuna ukatili wa aina nyingi akiutaja Mkoa wa Arusha kuongoza kwa vitendo vya ukeketaji.
Maadhimisho haya yanafanyika kufuatia mauaji ya watoto zaidi ya 2,000 yaliyofanyika katika kitongaji cha SOWETO Nchini Afrika ya Kusini mwaka 1976 yaliyosababishwa na Polisi wa Serikali ya Makaburu ya wakati huo walio kuwa wanaandamana kupinga mfumo wa utoaji elimu wa kibaguzi uliokuwa unawakandamiza watoto wa kiafrika ambapo hufanyika Tarehe 16 Juni kila mwaka lakini kwa mwaka huu yamefanyika Tarehe 13 Juni kutokana na ratiba ya serikali kuingiliana na sikuu ya Eid El Fitr.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa