Na Mwandishi Wetu,
Arusha.
Mkurugenzi wa Jiji la Arush Dkt John Pima amewataka wananchi wa jiji hilo kutoa ushirikiano kwenye zoezi la uwekaji wa anauni za makazi ambalo limeanza jana na linatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu na kwamba zoezi hilo ni bure kwani mwananchi hatagharimia chochote.
Akizungumza katika kipindi maalum kwenye kituo cha Radio Five kilichopo Jijini hapa Dkt Pima ametaja baadhi ya faida zitokanazo na anuani hizo ambazo ni kumtambulisha kila mwananchi popote pale alipo, kurahisisha huduma za kijamii kumfikia kwa kila mwananchi, kuondoa migogoro ya ardhi na mipaka miongoni mwa wananchi na na pia itasaidia kukuza sekta ya utalii.
Akifafanua juu ya ukuzaji wa sekta ya utalii amesema watalii wapata huduma watakazohitaji kwa wakati na urahisi na pia watafika popote watakapo bila kubabaika hali itakayopelekea watalii wengi kufika katika jiji la Arusha hivyo kuongeza kipato na ajira kwa wananchi wake.
“Kwa jiji la Arusha zoezi hili siyo geni kwani lilianza tangu mwaka 2008 chini ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, na hata 2018 lilianza tena lakini safari hii Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kulianzisha upya rasmi na ametenga shilingi bilioni 28 kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo nchi nzima ambapo pia litatoa ajira kwa vijana” Alisema Dkt Pima.
Amesema leo Jiji la Arusha litaendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wote wa Kata 25 ambapo kesho zoezi kama hilo la kuwajenga uwezo litafanyika kwa watendaji wa Mitaa, Wenyeviti wa Mitaa, wazee maarufu, na viongozi wa dini ili na wao waweze kutoa elimu sahihi kwa wananchi wao lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa zoezi linafanyika kwa ufanisi mkubwa ili kutimiza lengo lililokusudiwa.
Amesema zoezi la kutambua mitaa ambalo linashirikisha wananchi wote limeanza leo na linatarajia kumalizika baada ya wiki moja na kwamba wananchi wana wajibu wa kushiriki kikamilifu kwani zoezi hili ni lao na pia wananchi wana haki ya kubadilisha majina ya mitaa pindi wakiona kuna haja ya kufanya hivyo kwa kufuata maelekezo watakayopewa na wataalamu.
“Watendaji wa Kata, Mitaa na wenyeviti watakaa na wananchi wao kuwapa maelekezo, na niwaambie wananchi kuwa zoezi hili ya utambuzi wa mitaa na barabara ni lao, wao ndo wataamua kuwa mtaa huu au barabara hii iitwe jina gani” Alisema Dkt Pima.
Amesema wakati wa utekelezaji wa zoezi kwa maana ya kuweka namba za nyumba hakuna nyumba itakayorukwa kwani tayari ofisi ya Jiji ina wataalamu ambayo wana ramani inayoonyesha maeneo yote ya makazi pamoja na viwanja na pia namba hizo zitatolewa hata kwa kiwanja ambacho hakijajengwa au hakina hati.
“Kinachohitajika kutoka kwa mmiliki wa nyumba ua kiwanja wakati wa utekelezaji ni kitambulisho cha NIDA au namba ya NIDA kwa wale ambao hawajapata, kama mtu hana vyote atatoa kitambulisho chochote kinachotambulika, na mhusika atahitajika kutoa majina yake yote matatu……ni zoezi rahisi sana na halihitaji mambo mengi kutoka kwa mwananchi”
Aidha Dkt Pima amewataka wananchi kutunza miundombunu itakayowekwa kwa ajili ya kuweka namba za nyumba pamoja na nguzo za chuma zitakazotumika kuweka vibao vya majina ya mtaa na barabara kwani kuharibu miundombinu hiyo ni kuihujumu serikali na kwamba hatarajii wananchi kufanya hivyo kwani wakazi wa Jiji la Arusha ni watu wanaopenda maendeleo.
“Lakini niwaambie pia wananchi wa Jiji hili kuwa zoezi hili halitakwamisha shughuli zao za maendeleo, watu wataendelea na majukumu yao kama kawaida, kinachotakiwa ni kuacha vielelezo nilivyovitaja hapo juu kwa mtu yeyote atakayekuwa nyumbani siku hiyo ya zoezi ambayo mtaambiwa na watendaji wenu wa Kata na Mitaa” alisisitiza.
Aidha amewaambia wakazi wa Jiji hilo kuwa tayari serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)imeshatoa miongozo miwili itakayowarahisishia wananchi kujua kwa undani zoezi hili ambayo ni Muongozo wa Mfumo wa Anuani ya Makazi pamoja na Muongozi wa Post Code inayopatikana kwenye tovuti ya www.tamisemi.go.tz pamoja na tovuti ya www.arushacc.go.tz
Jana Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella alizindua zoezi la Mfumo wa Anuani ya Makazi kwa mkoa wa Arusha na kusisitiza ushirikiano wa wananchi kati zoezi hilo.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa