Katika muendelezo wa operesheni ya ukusanyaji wa mapato Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dr. Maulid Suleiman Madeni amefanya ziara ya kushtukiza katika Soko Kuu lililopo Jijini Arusha ambapo amewatembelea wafanyabiashara walioacha vibanda vyao ndani ya soko na kukimbilia nje kwa kisingizio cha kujifananisha na wamachinga.
Katika ziara yake hiyo aliyoifanya leo Tarehe 10/11/2018 Dr. Madeni amewakumbusha wafanyabiashara hao wajibu wao wa kulipa kodi ya serikali na ushuru wa vibanda kwani kwa kukimbia vibanda walivyotengewa kunaikosesha serikali mapato na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
(Pichani: baadhi ya biashara zinazoendeshwa kiholela nje ya Soko Kuu lililopo Jijini Arusha)
Pia amewataka wafanyabiashara hao ndani ya siku mbili wawe wamesharudi katika nafasi zao rasmi za awali kwani ndani ya soko idadi ya vibanda vilivyo wazi ni kubwa na kwa watakaokosa nafasi waonane na Afisa Bashara wa Jiji Bw. Godfrey Edward ili waweze kupangiwa maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya wafanyabiashara.
“Kwa kupanga bishara zenu kiholela mnasababisha kuzuia njia za waenda kwa miguu na sehemu za wateja kupaki vyombo vyao vya usafiri kitendo kinachosababisha usumbufu na ukosekanaji wa mapato hivyo niwaombe mrudi katika nafasi zenu za awali ili kuuweka mji wetu katika hali ya usafi” Alisema Dkt. Madeni
“Tunaelekea katika msimu wa mvua nyingi, tusipouweka mji wetu katika hali ya usafi na kuacha kuzuia biashara zinazipangwa kiholela basi tutayakaribisha majanga makubwa ya mlipuko wa magonjwa na uharibifu wa miundombinu kwani uchafu unaweza kuwa chanzo kikuu cha mifereji kuziba ” aliongeza Mkurugenzi huyo
Zoezi la kuwarudisha wafanyabiasha waliokimbia maeneo yao na kuvamia katikati ya Mji kiholela ni endelevu na Mkurugenzi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dr. Maulid Suleiman Madeni ataambatana na timu yake ya watumishi wa idara mbalimbali kuhakikisha wafanyabisahara wote wanapatiwa maeneo rasmi na kuuacha mji wa Arusha katika hali ya usafi kwani Jiji la Arusha ndio kitovu kikuu cha utalii.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa