Katika kutambua mchango wa wazee, Halmashauri ya Jiji la Arusha leo wamekutana na viongozi wa Baraza la Wazee Jiji la Arusha katika semina maalum yenye lengo la kuwajengea uwezo wa namna ya kuongoza Wazee wenzao katika maeneo yao na kutambua haki zao za msingi, semina iliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Arusha.
Akiongea na Viongozi hao, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dkt. Kheri Kagya amesema kuwa semina hiyo itawawezesha wazee hao ufahamu wa namna ya utekelezaji wa majukumu yao ngazi za kata na kwamba semina hiyo itawasaidia kuongoza na kuwatumikia vyema wazee wenzao katika maeneo yao.
Dkt. Kagya ameeleza kuwa semina hiyo ni muhimu kwani itawafanya wazee hao kufahamu namna Taasisi mbalimbali zilizomo ndani ya Jiji la Arusha zinavyofanya kazi kwani kufanya hivyo kutawawezesha viongozi hao wa wazee kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee waishio katika Kata zao.
Akiongea kwa niaba ya wazee hao, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Jiji la Arusha, Ndg. Mhina Sazua ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kuwapa elimu kwani awali hawakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu majukumu na taratibu za kazi zao na kwamba kwao ni faraja kuona Uongozi wa Halmashauri ya Jiji kukutana na wazee hao kwani kwao ni historia kukutana na kiongozi wa Serikali akisisisitiza kuwa hilo limewezekana kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu kupita tangu Baraza hilo lilipoanzishwa.
Naye Bi. Amina Yusufu, Mmoja wa washiriki Baraza la Wazee kutoka kata ya Ungalimited, amemshukuru Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. John Pima na timu yake ya wataalam kwa kulipa kipaumbele suala la Wazee na kwamba wazee ni hazina ya Taifa na kuwa wao ni vioo vya vijana wa sasa ambao ndio wazee wa taifa la Kesho.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa