Na Mwandishi wetu
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) ,Simon Sirro amewaagiza wenyeviti wa serikali za mitaa,watendaji kata na vijiji, kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kulinda amani na kutanguliza Uzalendo wa nchi ikiwa ni pamoja na kuwabaini wageni wanaoingia katika maeneo yao, ili kufichua wahalifu na magaidi kabla ya kufanya vitendo vya umwagaji damu na uporaji.
Kamanda Sirro ameagiza kupelekwa Askari Kata ili kuweza kukabiliana na kata zenye uhalifu na ukiukwaji wa haki za Binadamu.
Akizungumza mapema leo Jijini Arusha na watendaji kata,wenyeviti wa serikali za mitaa,viongozi wa dini na polisi Jamii, IGP Sirro alisisitiza lazima wenyeviti hao wahakikishe amani na utulivu unakuwepo katika jamii zao na kujiepusha kufumbia macho matukio ya kiuhalifu na wahalifu.
"Arusha imepakana na nchi jirani hivyo kuingia kwa wageni wasio na nia njema na nchi yetu ni rahisi wakitokea nchi mbalimbali kama Somalia au Msumbiji, lazima kila mmoja awe makini na wageni hao tuepuke matukio ya miaka iliyopita ya mabomu katika maeneo mbalimbali,"alisema.
Aidha aliwataka viongozi hao kutanguliza maslahi ya Taifa na wananchi badala ya maslahi yao kwakua mstari wa mbele kufichua wahalifu na uhalifu unaofanyika katika maeneo yao.
Alisema upo uwezekano wa baadhi ya wahalifu kirudi nchini na kufanya matendo ya kigaidi,hivyo ni Vyema kila mmoja akajipanga.
Alisema hali ya usalama kwa sasa nchini ipo shwari japo siku za karibuni kulianza kibuka matukio ya uhalifu kutokana na majambazi wengine kukata rufaa na kuachiwa huru na kuendeleza vitendo vya uhalifu
Pia aliagiza mikutano ya kila mwezi Kati ya Mkuu wa Polisi Wilaya(OCD) na viongozi wa ngazi mbalimbali za chini kwaajili ya kupeana taarifa za matukio mbalimbali na kuzitatua, kwani uhalifu unaanzia majumbani,mitaani na maeneo mengine.
"Tunahimiza ushirikiano na wananchi juu ya ulinzi shirikishi kwani bado polisi ni wachache ukilinganisha na idadi ya watanzania waliopo, hivyo ushirikiano ni muhimu katika kufichua na kukomesha matukio ya kiuhalifu,"alisema.
Pia IGP Sirro aliwaonya wanaojiingiza katika matukio ya uhalifu na ugaidi kuacha mara moja, kwani hawatasalimika pale watakapokamatwa na Polisi na hakuna wa kumlaumu pale watakaposhughulikiwa.
Akizungumza kuhusu madawa ya kulevya alisema Arusha ni Mkoa wa pili au tatu, kwa uuzaji wa madawa ya kulevya hivyo ni aibu kwa viongozi waliopo sababu lazima wanawafahamu na kuwafumbia macho.
Alisema ni lazima hatua zichukuliwe ili kudhibiti matukio hayo na kusisitiza uimarishaji wa doria katika maeneo husika, ili kudhibiti suala hilo la madawa ya kulevya hasa katika Kata ya Ungalimited.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Arusha,Sophia Mjema alisisitiza umuhimu wa ulinzi na usalama ngazi za chini ili kuleta amani na utulivu katika kila kata na serikali za mitaa.
Wakati huo huo,Mbunge wa Arusha Mjini,Mrisho Gambo alisema Arusha ni Jiji la Utalii lakini huwezi kufanya utalii bila kuwa na amani.
Mh .Gambo aliahidi kutoa Sh. milioni 5 kwa ajili ya kituo cha Polisi Olasiti ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dk.John Pima alisema kuwa Uongozi wa Halmashauri utahakikisha Ujenzi huo unakamilika na kwa kuanzia watangia Tshs million 5 na kwamba kujengwa kwa kituo cha polisi kitasaidia kudhibiti Uhalifu .
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa