Halmashauri ya jiji la Arusha imetia saini mkataba wa mradi wa huduma ya ushauri katika utafiti na usanifu wa mfumo wa utiririshaji wa maji ya mvua kwa ajili ya maandalizi ya mpango kabambe wa uboreshaji wa mifumo ya mitaro ya maji ya mvua na maji taka katika jiji la Arusha kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020 hadi 2040.
Mradi huo unaojulikana kwa jina la Drainage and Sanitation System Project (DSDP) wenye gharama ya fedha za kimarekani (USD) 647,463.00 upo chini ya utekelezaji wa mradi mama wa Uboreshaji wa Miji na Majiji Nchini (TSCP) awamu ya pili na umesainiwa Tarehe 06/05/2019 na Mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt. Maulid Suleiman Madeni akishuhudiwa na Mstahiki Meya wa Jiji Mhe. Kalisti Lazaro . Mradi huu wa mwaka mmoja unatekelezwa na kampuni ya mhandidi mshauri ya Cheil Engeneeting Co.Ltd kutoka nchini Korea iksishirikiana na AJOMA Limited kutoka Tanzania.
Wakati wa hafla fupi ya kusainiwa kwa mkataba huo, Mratibu wa miradi ya TSCP jiji la Arusha, Mhandisi Agust Mbuya amefafanua malengo makuu ya mradi huo kuwa ni kuandaa mpango jumuishi wa mifumo ya maji ya mvua na maji taka ambao utahusisha mifumo ya maji ya mvua, ukusanyaji wa maji taka kutoka kwenye ngazi ya kaya, usafirishaji salama kutoka kwenye makazi, uhifadhi pamoja na uchakataji kwa lengo la kubadili maji taka kuwa bidhaa nyingine kwa matumizi anuai yenye tija na salama kwa jamii.
“Tunatarajia kuwa kazi hii ya usanifu itatupatia mpango wa utekelezaji kwa awamu kwa kipindi cha miaka 20 kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2040 na pia usanifu huo utatupatia mwelekeo wa mfumo bora wa usimamizi katika ujenzi, kuendeleza na kutunza mifumo hiyo ya maji ya mvua na maji taka katika jiji letu” alisema mhandisi huyo.
Pia aliongeza kuwa lengo la pili la kazi hiyo ya usanifu ni kupendekeza mradi wa awali utakaoweza kufanyika kwa misimu ya miaka mitano mitano kuanzia mwaka 2020. Mradi wa miaka mitano wa awali uainishe maeneo yasiyopungua matano yanayotakiwa kuanza utekelezaji na kuwasilisha nyaraka za awali za michoro ya usanifu, makisio ya gharama pamoja na zile za zabuni zitakazowasilishwa kwa wahisani kwa ajili ya ufadhili.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. Maulid Suleiman Madeni alisema kuwa ni matarajio yetu kama halmashauri kuwa usanifu huu utatupa suluhisho la kudumu katika kupambana na mafuriko ya mara kwa mara ndani ya jiji la Arusha pamoja na kuweka mfumo thabiti wa ukusanyaji wa maji taka ili kuhakikisha mazingira ya jiji yanabaki kuwa nadhifu na salama kwa wananchi wetu.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa