Na Mwandishi Wetu
Arusha
Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maximilian Matle Iranqhe amewataka wafanyabiashara wadogo maarufu Kama Machinga Jijini Arusha kuiamini Serikali kwakua inawajali na kuwatatulia changamoto zinazowakabili ikiwemo miundombinu ya masoko na kwa kuanza wameshamwaga na kusambaza moramu katika baadhi ya masoko kama Machame Luxury, Namba 68, Soko la Kilombero, Samunge na mengineyo.
Mhe. Iraqhe alitoa wito huo Mei 21, 2023 wakati alipotembelea na kukutana tena na machinga hao katika soko la Machame Luxury lililopo Jijini Arusha kwa lengo la kufuatilia na kushuhudia utekelezaji wa ahadi ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili machinga ambazo Meya Iranqhe aliahidi kuzifanyia kazi wiki mbili zilizopita alipotembelea masoko hayo.
Pia, alimwomba Mwenyekiti wa Soko hilo kuwaunganisha pamoja wafanyabiashara wa soko hilo na asiruhusu mtu yeyote kuwagawa wamachinga hao pamoja na kushirikiana na Serikali nakuongeza kuwa yale yote walioahidiwa watatekelezewa.
"Niwaombe muiamini Serikali yenu, niwaombe muwaamini viongozi wa wamachinga kwenye soko hili lakini machinga Wilaya lakini pia mumuamini Mkuu wenu wa Wilaya, Mbunge, Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi hawa wote wanafanyakazi chini ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kwa hiyo wote tunajenga nyumba moja tusigombalnie fito " alisema Iranqhe.
Aidha, alibainisha kuwa wanataka Jiji la Arusha liwe Jiji la kwanza kwa kujiendesha lenyewe kwa mapato ya ndani ndio maana Serikali inajenga masoko ya kimkakati.
"Ninaomba kila mtu aamini Serikali tuko hapa kwa ajili ya kutatua matatizo yenu kutatua changamoto zenu na kuhakikisha maisha yenu yanapanda maana yake ukiwa kijana unaweza kuwa machinga hapa na pale lakini ukiwa mtu mzima huwezi kuwa machinga Sasa lengo la Serikali nikuwaanda kutoka kwenye umachinga kwenda kwenye wafanyabiashara wa kati, wafanyabiashara wakubwa na mimi naamini hii inawezekana tukishirikiana kwa pamoja " alisema Meya Iranqhe.
Aidha aliongeza kuwa katika asilimia kumi ya mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Arusha Wanataka kuwapatia mikopo wamachinga ili watoke kwenye umachinga na kwenda kuwa wafanyabiashara.
Kwa upande wake kiongozi wa machinga Wilaya ya Arusha, Idrisa Chongoza aliishukuru Serikali na viongozi wa Jiji hilo akiwemo Mstahiki Meya na Mkurugenzi wa wa Jiji hilo kwa kuwatatulia changamoto zinazowakabili ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya masoko.
"Nawaombeni sana wafanyabiashara wenzangu tulieni kwa sababu Serikali inapokuja kutekeleza majukumu yake ikiwakosa tena eti mko barabarani mnahangaika hasa itakuwa inamtengenezea nani sisi wafanyabiashara tujikague wenyewe tukae Sasa kwenye maeneo yetu ya biashara tuhakikishe tunatulia Serikali imeshaanza kufanyakazi Arusha yetu itatulia maisha yataendelea " Alisema Chongoza.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa