Na Mwandishi Wetu,
Halmshauri ya Jiji la Arusha limemuunga mkono kwa vitendo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kukabidhi mahitaji ya shule kwa wanafunzi zaidi ya mia nne waliotoka katika familia duni hali iliyopelekea kushindwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Baraza la madiwani, watumishi, watendaji pamoja na wadau wa maendeleo waliopo ndani ya Jiji hilo wamefanikiwa kutoa sare za shule kwa wanafunzi 413, madaftari, kalamu, penseli, rula pamoja na taulo za kike.
Vifaa vingine ni pamoja mabegi kwa ajili ya kubebea madaftari, pea za viatu pamoja na soksi na kwamba zoezi hilo limefanikiwa kwa asilimia 104 kwa maana ya kupata mahitaji ya ziada.
Mgeni rasmi katika hafla ya kuwakabidhi wanafunzi mahitaji hayo iliyofanyika katika shule ya sekondari Naura iliyopo Halmashauri ya Jiji hilo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda ameipongeza halmashauri ya Jiji hilo kwa kubuni wazo zuri ambalo amesema hiyo ndiyo maana halisi ya kumuunga mkono Rais katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuhakikisha kuwa watanzania wanapata huduma bora.
“Mhe Rais anataka kila mtanzania apate huduma bora ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa sera ya elimu bila malipo inamgusa kila mwanafunzi kwa maana ya wenye uwezo na wasio kuwa na uwezo wa kumudu mahitaji ya shule kama vile sare za shule, madaftari, kalamu, taulo za kike nk, hivyo kwa hatua hii iliyofikiwa na jiji nina imani kuwa hakuna mtoto atashindwa kuripoti shuleni kutokana na changamoto hizi” Alisema Mkuu wa wilaya.
Aidha amewaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao kwa kuwa serikali yao inaendelea kuboresha mazingira ya shule na kusisitiza kuwachukulia hatua wazazi ambao watoto wao hawataripoti shule huku akiahidi kuendelea kutoa motisha kwa walimu ikiwemo ujenzi wa nyumba zao ili kuwapunguzia changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda makazini mwao.
“Hii sasa ndiyo maana halisi ya kumuunga mkono Rais wetu Mhe. Samia, niwapongeze sana Jiji kwa kuanzisha hii programu na niwasihi iwe endelevu kila mwaka, na mimi nawaahidi kushirikiana nanyi bega kwa bega……lakini nitoe rai kwa wazazi kuhakikisha kuwa watoto wa darasa la kwanza wanaandikishwa shule na wa kidato cha kwanza wanaripoti shule, kwa mzazi ambaye hatazingatia agizo hii muda wa kuripoti na kuandikishwa shule ukipita tutamchukulia hatua” Alisema Mkuu wa wilaya.
Katika uchangiaji huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Arusha Dkt John Pima ametoa sare za shule kwa wanafunzi wote 413 ambapo amewataka wana Arusha kuungana ili kufanya kitu kikubwa zaidi na kuhakikisha hakuna mwanafunzi wenye sifa ya kusoma anashindwa kwa sababu ya kukosa mahitaji.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema Jiji la Arusha kwa kushirikiana na Baraza la madiwani limedhamiria kufuta daraja la sifuri kwa kutenga fedha kiasi cha shilingi milioni 98 kwa ajili ya kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wa kidato cha pili na nne watakaopata daraja A katika masomo yao.
“Zoezi hili limefanyika si chini ya mwezi mmoja, lakini tumefanikiwa kukusanya mahitaji haya kupita malengo tuliyojiwekea, hii inaonyesha kuwa iwapo wana Arusha tutaungana tutafanya kitu kikubwa sana zaidi ya hili na tunakuwa tunamuunga mkono Rais wetu mama Samia kwa vitendo” Alisema Dkt Pima.
Mstahiki Meya wa Jiji hilo Mhe. Maximilian Iranqhe amesema katika kuhakikisha kuwa Jiji hilo linakuwa la mfano kwa majiji yote nchini kwenye idara zote pia wametenga kiasi cha shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya kujenga madarasa mapya katika za sekondari Unga Ltd pamoja na shule ya sekondari Kalimaji pamoja na kuongeza vyumba vya madarasa ya ghorofa katika shule nne za sekondari za Jijini humo.
“Mazingira mazuri ya kujifunza na kujisomea yamechangia kwa kiasi kikubwa ufaulu wa wananafunzi kwa mfano matokeo ya mwaka huu ya kidato cha nne yamepanda hadi kufikia wastani wa asilimia 92.5 kutoka wastani wa asilimia 87.5 mwaka jana, lakini pia ufaulu wa kidato cha sita mwaka jana umepanda hadi kufikia wastani wa asilimia 99” Alisema Mstahiki Meya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Mhe. Mrisho Gambo amepongeza zoezi hilo ambalo limetatua changamoto ya watoto walioanza kukata tamaa ya kukosa masomo kutokana na changamoto ya ugumu wa maisha kwenye familia zao na kuahidi kutoa madaftari 500 pamoja na taulo za kike 50 kwa muda miezi sita.
Baadhi ya wanafunzi wanufaika wa mpango huo, Frank Nyandwe na Lulu Hillary wameishukuru halmashauri ya jiji ya Arusha kwa kuona dhamani ya kila mwanafunzi kupata elimu na kuamua kuwasaidia mahitaji hayo na kuahidi kusoma kwa bidii ili watimize ndoto zao.
Mhe. Maxmillian Iranqhe
Mstahiki Meya Jiji la Arusha
Dkt. John Pima
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa