Na Mwandishi Wetu
Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maxmillian Matle Iranqhe amesema kuwa Jiji la Arusha imeendelea kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato ambapo robo ya kwanza ya Mwaka halmashauri hiyo imekusanya zaidi ya asilimia 25 ambapo ni sawa na zaidi ya sh.bilioni saba ambapo fedha hiyo imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Mstahiki Meya ameyasema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Baraza la Madiwani robo ya kwanza ya Mwaka wa fedha 2022 /2023 uliofanyika Novemba 08, 2022 na kusema kuwa fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
"Tumeielekeza katika ujenzi wa madarasa zaidi ya 100 ya sekondari na msingi,pia watajenga na kuboresha vituo vya afya ,Ofisi za kata,uboreshaji wa miundombinu ya barabara za kiwango cha lami,"alisema Iranqhe.
Alisema wakazi wa Jiji la Arusha wategemee maendeleo makubwa katika robo hii ya mwaka ikiwa hata ndani ya mwezi Oktoba wameshakusanya takribani sh.bilioni 2.7.
"Pia katika fedha hizo nguvu kubwa tutaielekeza katika taa za barabarani kwani mji wa Arusha kwenye nyakati za usiku kunakabiliwa na changamoto ya giza pamoja na huduma ya umeme kukatika pia wamebaini taa hizo haziwaki katika kipindi cha usiku,"alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Hargeney Chitukuro alitoa wito kwa watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuzingatia kufanya kazi kwa wito na nidhamu ya hali ya juu katika kutoa huduma kwa wananchi.
"Kwa upande wa wauguzi ambao wanatoa lugha chafu kwa wagonjwa namuelekeza Afisa Utumishi wa Halmashauri hii kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine na ikumbukwe kazi ni wito,"alisema Chitukuro.
Nao baadhi ya madiwani walilishauri Jiji hilo kuendelea kutoa elimu kwa watumishi wa umma kuzingatia weledi na sheria za kazi katika utoaji wa huduma kwa wananchi hasa sekta ya afya.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa