Kamati ya Fedha yafanya maamuzi magumu, yaagiza ukarabati wa soko la kilombero kufanyika haraka
Na Mwandishi wetu.
KAMATI ya Fedha ya Halmashauri ya Jiji la Arusha imeagiza kufanyika kwa ukarabati wa miundo mbinu katika soko la bidhaa za biashara la kilombero ikiwa ni pamoja na kumwaga na kusambaza Moramu katika maeneo yaliyoharibiwa vibaya na Mvua pamoja na kuzibua mifereji na kuezeka paa za nyumba za biashara ambazo zimeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kamati hiyo imetoa agizo hilo baada ya kutembelea na kuona uhalisia wa maeneo ya Biashara katika soko la Kilombero na pia baada ya wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo hatarishi kutoa kilio mbele ya kamati hiyo wakieleza adha wanayopata na kuomba Serikali kuchukua hatua kabla hawajapata madhara ya milipuko ya magonjwa ikiwa ni pamoja kuwatafutia eneo la biashara.
Eneo hatarishi kuliko yote ni eneo walipofanyabiashara wa samaki ambao wanasafisha na kuparua samaki katikati ya madimbwi ya maji ya matope ya mvua bila kujali mlipuko wa mgonjwa.
Kamati hiyo ikiwa inayoongozwa na Meya wa Jiji la Arusha Maxmilian Iranqhe inaagiza wataalam wa Halmashauri wa Jiji la Arusha wakiongozwa na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kufanya ukarabati wa miundo mbinu hiyo na kuweka Moramu katika maeneo hatarishi pamoja kuzibua mifereji.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk.John Pima anaelezea zoezi hilo na kudai kuwa wameanza utekelezaji na kuwataka wafanyabiashara kuwa wavumilivu huku wakifuata sheria na taratibu .
Dk.Pima pamoja na mambo mengine anawataka wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga kufuata taratibu huku wakisubiri zoezi la ukarabati kufanyika na baada ya ukarabati utaratibu utafanyika ili kuweza kupanga wafanyabiashara kulingana na taratibu lengo ikiwa ni kulinda afya za watu na maisha ya watu.
Anasema kuwa Serikali inajali afya za watu na dhamana ya maisha ya watu iko mikononi mwa Serikali kuwa tahadhari kabla ya hatari ni bora kuliko kusubiri hatari.
Anawakumbusha wafanyabiashara maarufu kwa jina la Wamachinga kwenda kujiandikisha ili waweze kupata kitambulisho na kurasimisha biashara zao w na kuwatenga na wafanyabiashara wakubwa wanaojiita wamachinga wakati hawana sifa ya kuitwa Machinga.
Ametaja vituo vya kujiandikisha kuwa ni Makao makuu ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, Kata ya Levolosi Kata ya Themi, kata ya Muriet na kuwa katika vituo hivyo kuna wataalam wanaotoa maelekezo ya jinsi ya kujiandikisha.
Kimsingi anasema kuwa wafanyabiashara ambao hawatajiandikisha watahesabiwa kuwa ni wafanyabiashara wakubwa wataingia katika orodha ya wafanyabiashara wanaotakiwa kuchukua leseni za biashara.
Hata hivyo anasema kuwa Serikali imechukua hatua kwa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara ambao hawana mahali pakufanyia kazi zao na kwamba wataoneshwa maeneo hayo lengo ikiwa ni kuwawezesha kufanya kazi katika mazingira salama ambayo hawezi kuhatarisha maisha yao.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa