Na Mwandishi Wetu
Kamati ya huduma za jamii(Uchumi, Elimu na Afya) ya Halmashauri ya Jiji la Arusha imewataka Maafisa maendeleo ya jamii wa Jiji hilo kutoa elimu ya kutosha kuhusu mikopo ya asilimia kumi ili kila mlengwa aweze kunufaika.
Akizungumza Jijini Arusha, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Isaya Doita alisema ni vyema Maafisa mendeleo ya jamii wakahakikisha wanaweka mikakati mizuri ya utoaji elimu kwa wananchi waelewe utaratibu wa uchukuaji wa mikopo pasipo kuwa na vikwazo vyovyote vinavyoweza kuwakwamisha kuchukua mikopo hiyo ya halmashauri.
"Elimu ya mikopo hiyo ikitolewa kuanzia ngazi ya viongozi wa mitaa itasaidia kuongeza tija katika makundi ambayo yanahitaji mikopo hiyo kwa ajili ya kujiendeleza na kukua kiuchumi,"Alisema Doita ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ngarenaro.
Aliongeza kuwa fedha nyingi mikopo ya asilimia 10 zinapotea kutokana na baadhi ya walengwa kukosa elimu na taarifa katika halmashauri hiyo hazionyeshi maendeleo yoyote hivyo ni wajibu wa Maafisa maendeleo kufuatilia ili kuleta tija ya mikopo hiyo.
"Ni wajibu wa Maafisa maendeleo wa wilaya ya arusha kufuatilia maendeleo ya wanufaika wa mikopo hiyo ili kuleta tija ,"alisema Doita.
Awali Mhe. Doita aliisifu Halmashauri ya Jiji la Arusha kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuja na mkakati wa 'City Mobile Training Unity' kwa maana ya kufikisha huduma kwa jamii ya wananchi ambalo kwa kuanzia limenzia katika kata ya Terrat na kusema kuwa zoezi hilo ni zuri na lenye tija na kusisitiza kuwa liwe endelevu kwa manufaa ya wananchi wote wa Jiji la Arusha.
Kwa upande wake,Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii,Shabani Manyama alisema sekta zote zinahitajika kushusha huduma kwa jamii katika kuwa na umiliki kwenye miradi iliyotekelezwa katika maeneo yao ili kuleta tija ya serikali kuwekeza fedha.
"Na ndio maana mahali popote ambapo hakuna nguvu za wananchi hatuleti maendeleo kwani lazima waweke nguvu zao katika utekelezaji wa miradi ili waweze kuona uchungu wa kuilinda,"alisema.
Mmoja wa wakazi wa jiji la Arusha,Grace Kivuyo aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Arusha kuanzisha mkakati wa utoaji wa elimu kupitia vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kwani walikuwa wanapata adha ya kukosa mikopo kutokana na kushindwa kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa