Nteghenjwa Hosseah - Arusha
Shule ya msingi Lucky Vicent yaibuka na mshindi wa Jumla Kitaaluma kwa kushika nafasi ya kwanza Kimkoa katika maadimisho ya Juma la Elimu yaliyoadhimishwa katika viwanja vya Arusha School jijini hapa.
Shule hiyo iliyopata na msiba wa wanafunzi 32, walimu 2 pamoja na dereva kutokana na ajali ya Coastal hivi karibuni imefanya vizur katika mitihani ya darasa la saba iliyofanyika mwaka 2016 katika ngazi ya Mkoa na Wilaya hivyo kujinyakulia Kombe pamoja na Cheti.
Akipoka zawadi hizo za Ushindi Mwel Mkuu wa Shule hiyo Bw. Innocent Mushi alisema wanafarijika kupata zawadi hizo ingawa bado simanzi na majonzi yametanda shuleni kwa wanafunzi pamoja na uongozi wa shule hiyo.
“Tunamshkuru Mungu kwa Shule yetu kufanya vizuri na hizi ni jitihada za walimu kufanya kazi kwa bidii pamoja na wafunzi kuzingatia yale wanayofundishwa na walimu wao hakika zawadi hizi zimetupata faraja katika kipindi hiki kigumu tunachopitia.” Alisema Mwl. Mushi.
Katibu Tawala wa Jiji la Arusha Ndg. David Mwakiposa ambaye ndiye mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amepongeza shule zote zilizofanya vizuri Kitaaluma kwa mwaka uliopita ikiwa ni pamoja na Walimu na Wanafunzi na pia alitembelea miradi ya kiubunifu inayoendeleza sanaa za wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kupata ajira hapo baadae.
Mwakiposa alisema “Taifa lolote haliwezi kuendelea pasipo wananchi wake kuelimika hivyo nichukue fursa hii kuweka msisitizo kwa walimu na viongozi mbalimbali katika sekta ya elimu kufundisha wanafunzi kwa weledi na kutoa elimu bora ili malengo mbalimbali ya kitaaluma yaweze kufikiwa”
Pia aliongeza kwa kusema kuwa amefurahishwa na kuhamasishwa sana katika maonyesho yaliyofanywa na wanafunzi hasa maonyesho ya mafunzo ya kitaaluma, kisayansi na ufundi stadi na kusisitiza kuwa endapo watashirikisha jamii taaluma walizofundishwa na walimu wao na wakiwezeshwa na wadau wa elimu basi Tanzania yetu itapiga hatua kubwa hasa katika suala zima la uchumi wa viwanda.
Miongoni mwa maonyesho yaliyoweza kuonyeshwa na wanafunzi wa kawaida na wenye ulemavu ikiwemo viziwi, matatizo ya akili na wasioona ni pamoja na utaalamu wa kusindika maparachichi na kutengeneza mafuta yanayoweza kutumika kama kilainishi katika karakana za vyuma vyenye kutu na dawa ya ngozi, ujuzi wa kutengeneza dawa ya kung’arishia viatu pamoja na ushonaji wa nguo na vitambaa vya kupambia majumbani.
Pia wanafunzi walionyesha namna ya kuzalisha umeme kwa kutumia nyaya, utengenezaji wa mapambo kwa kutumia shanga zinazotokana na makaratasi na watoto wenye ulemavu wa kusikia wanavyoweza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)katika kujifunza mambo mbali mbali.
Maadhimisho ya Juma la Elimu hufanyika kila mwaka lengo ikiwa ni kutathimini ubora wa Elimu, kuwatambua waliofanya vizuri kitaaluma na kuonyesha kwa vitendo ubunifu wa wanafunzi na sanaa inavyokua katika sekta ya Elimu.
Mwisho
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa