Maafisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri Jiji la Arusha watakiwa kutoa elimu kwa makundi maalum
Na mwandishi wetu
MAAFISA Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Arusha wametakiwa kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vya akina mama, vijana na walemavu ambao wanasifa ya kupata mkopo wa asilimia 10 mikopo ambayo inatolewa kupitia mapato ya ndani ya kila Halmashauri nchini, Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwa miongoni mwa Halmashauri hizo, yakiwa ni maagizo ya Serikali.
Lengo la kutolewa kwa mikopo kwa makundi hayo ni kuwawezesha kuanzisha shughuli za kujikwamua kiuchumi na hatimaye kuupa umaskini kisogo.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk.John Pima ametoa maagizo kwa maafisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri hiyo kutoa elimu sahihi kwa walengwa ili waweze kupata mikopo na kuanzisha miradi yenye tija .
Dk. Pima anasema kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha imefanya vizuri katika kutoa mikopo kwa walengwa lakini imebainika kuwa baadhi ya wanakikundi wameshindwa kuanzisha miradi yenye tija na baadhi ya wanakikundi wamebainika kutumia fedha hizo kinyume na malengo .
Mwanamsiu Dossi ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Arusha anasema kuwa tayari wameanza kutoa elimu katika kata 25 kwa makundi yaliyoainishwa na yenye sifa ya kupewa mkopo na kwamba nia ya wataalam ni kuona maisha ya watu yanabadilika na kuwa bora Zaidi .
Kimsingi alisema kuwa wamefurahi kukumbushwa maagizo ya Serikali ya namna na kwamba wataendelea kutoa elimu ili kuwezesha walengwa kubuni na kuanzisha miradi bora na hatimaye kuondokana na umaskini .
Dossi alisema kuwa wanatarajia kuona maisha bora na mapinduzi makubwa ya maendeleo ikiwa wananchi na walengwa wa mikopo hiyo watapokea elimu na ushauri kutoka kwa wataalam wanaopatia elimu juu ya namna bora ya kutumia mikopo watakayopata .
Kwa upande wao maafisa hao wa maendeleo ya jamii wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa elimu kwa walengwa wa mikopo hiyo inahitajika na kudai kuwa wataendelea kutoa elimu bila kuchoka ili kupata miradi yenye tija na hatimaye kuwezesha wahusika kuondokana na umaskini .
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa