Baraza la madiwani la Halmashauri ya jiji la Arusha mapema hapo jana limefanikiwa kuketi kikao cha robo ya tatu kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya jiji la Arusha.
Wakati akifungua kikao hicho Mstahiki Meya wa jiji la Arusha ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza la madiwani, Mhe. Kalist Lazaro Bukhay amewapongeza watumishi kufuatia jiji la arusha kupata hati safi kwa miaka minne (4) mfulululizo kufuatia ripoti ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) iliyotolewa hivi karibuni.
Katika ufunguzi wa kikao hicho Mhe. Kalist Lazaro alisema kuwa hapingani na zoezi la utoaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo (machinga) katika jiji la Arusha isipokuwa zoezi hilo limeathiri ukusanyaji wa mapato kwani baadhi ya watumishi wamekuwa wakigawa vitambulisho hivyo kwa wafanyabiashara walio na mikataba ya kisheria na Halmashauri.
Akiongeza katika hilo ametolea mfano wa makusanyo yalivyokuwa kabla na baada ya zoezi la vitambulisho kuanza katika soko la NMC, alisema kuwa soko hilo lina vizimba 2640 na mapato yalikuwa ni shilingi milioni 21 kwa mwezi lakini hadi kufikia juzi ni wafanyabiashara wenye vizimba 40 tu ndio hawana vitambulisho hivyo kupelekea mapato kushuka hadi shilingi 10,000/= kwa siku.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt. Suleiman Madeni amekiri changamoto hiyo kwani kwa nyakati tofauti amekuwa akipokea simu kutoka kwa wakuu wa masoko wakilalamikia baadhi ya watumishi kugawa vitambulisho ndani ya masoko.
“Nimesikitishwa sana na kitendo cha baadhi watumishi wa Jiji hili kugawa vitambulisho kwa wafanyabiashara wasiostahili kwani kufanya hivyo ni kuhujumu mapato ya Halmashauri na pia ni kuenda kinyume na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli” alisema Dkt. Madeni
Kufuatia ajenda hiyo ya dharura iliyoanzishwa wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Mstahiki meya wa jiji la Arusha Mhe. Kalist Lazaro Bukhay amewataka wataalam wa Halmashauri kuandaa taarifa ya kitaalamu itakayoonyesha hali halisi ya zoezi hilo, athari za ugawaji wa vitambulisho katika vyanzo vya mapato, ushauri wa menejimenti na kupitia upya sheria za mapato za serikali za mitaa ili kuepuka hoja za ukaguzi na hati chafu.
Katika kikao hicho pia maazimio mbalimbali yaliweza kutolewa ikiwemo suala la kutenga bajeti za kata kwa ajili ya maboresho muhimu ya miundombinu ambapo Mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt. Maulid Suleiman Madeni amesema kwakuwa bajeti ya mwaka huu wa fedha ilishapitishwa hivyo amewaomba madiwani na maafisa watendaji wa kata kuwasilisha taarifa za maboresho ya miundombinu katika maeneo yao ya utawala kwa ajili ya kutengewa fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao, 2019/2020.
Aidha kikao hicho cha baraza la Madiwani kilipokea taarifa mbalimbali kutoka katika taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zinazotoa huduma kwa wananchi wa Jiji la Arusha.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa