Msimamizi wa uchaguzi mdogo jimbo la Arusha Mjini ndg. Athumani kihamia amezindua rasmi mafunzo ya makarani waongozaji wapiga kura watakaoshiriki katika zoezi la uchaguzi mdogo wa madiwani kata ya Murriet ifikapo Tarehe 26.11.2017, jijini hapa. Mafunzo hayo yamezinduliwa rasmi mapema leo hii katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
“Mmepata nafasi hii ya kuwa makarani waongozaji wapiga kura kwa kuwa mna uwezo mkubwa wa kuwaongoza na kuwasimamia ipasavyo wapiga kura bila kuvunja sheria elekezi ya Tume ya Uchaguzi hivyo nina imani mafunzo mliyopatiwa leo mtayatekeleza vyema” . Alisema msimamizi wa uchaguzi huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa jiji la Arusha.
Aidha msimamizi huyo wa uchaguzi amewataka makarani waongozaji wapiga kura kutojihusisha au kushabikia chama chochote cha siasa jambo litakalopelekea kuharibu uchaguzi huo vilevile kuepuka hali yoyote ya upendeleo wa kiitikadi.
Pia amewataka makarani wote kuwa waadilifu katika kuwaongoza wapiga kura siku hiyo ya tarehe 26/11/2017 kwa kufata kanuni na sheria za uchaguzi na pia kuwa waaminifu kwa kuficha siri za uchaguzi huo.
Afisa Utumishi Ofisi ya Rais, Bi. Tausi Moshi pia alipata fursa ya kuongea na makarani waongozaji wapiga kura ambapo alitoa onyo kwa makarani hao kutojihusisha na vitendo vya rushwa ama vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani kwani vipo nje ya maadili na vinaweza kuharibu kwa kiasi kikubwa zoezi hilo la uchaguzi.
Semina kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Madiwani kata ya Murriet jijini Arusha imekamilika kwa makarani waongozaji wapiga kura na itaendelea siku ya kesho Tarehe 23.11.2017 kwa wasimamizi wasaidizi wa vituo vya uchaguzi katika ukumbi wa mkuu wa mkoa saa mbili kamili asubuhi.
MWISHO.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa