Na Mwandishi Wetu,
Arusha.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt John Pima amesisitiza umakini kwenye zoezi la uingizaji wa namba za majira ya nukta linalotarajiwa kuanza kesho mara baada ya kukamilika kwa zoezi la utambuzi wa anwani za makazi kwenye Kata tano za jijini hapa zoezi ambalo linatarajiwa kumalizika leo.
Akifungua mafunzo ya namna ya kutumia mfumo wa kidigitali wa anwani za makazi(NAPA) kwa vijana 54 wanaofanya kazi za usajili, Mkurugenzi huyo amesema zoezi hili ni nyeti sana hivyo linahitaji utulivu na umakini wa hali ya juu.
Licha ya kusisitiza umakini wakati wa kuingiza namba za majira ya nukta, aidha aliwasisitiza kuwepo kwa mawasiliano ya mara kwa mara na ya haraka pamoja na kutoa huduma bora kwa wanaowahudumia.
“Naomba umakini wa hali ya juu, iwapo hili halitazingatiwa ni wazi kuwa tutatoa namba ambazo zitakuwa siyo sahihi na hazitambulishi eneo husika, kwa maana hiyo eneo husika halitatambulika kwenye mfumo” Alisema Dkt Pima na kuongeza.
“Epukeni kujiongeza, mkiona changamoto yoyote msisite kuwauliza wataalamu wetu ambao mtakuwa nao kwenye zoezi na ndiyo maana nawasisitiza kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na ya haraka ili kuweza kutatua changamoto yoyote itakayojitokeza”
Aidha Dkt Pima amewapongeza vijana hao kwa kufanya kazi nzuri kwenye zoezi la kuweka namba za utambuzi wa anwani za makazi na kuwataka kuendela kujituma kwenye zoezi la kutumia mfumo wa NAPA kwa kuhakikisha wanaonyesha taswira nzuri ya serikali kwani wanafanya kazi hiyo kwa niaba ya serikali.
Zoezi la utambuzi wa anwani za makazi kwenye Kata hizo limeendeshwa mwa muda siku mbili na linatarajiwa kumalizika hii leo ili kuingia kwenye hatua ya uwekaji wa majira ya nukta yaani Code Net.
Mafunzo ya kutumia mfumo wa NAPA kwenye Kata tano za Kaloleni, Levolosi, Themi, Sekei pamoja na Kata ya Kati yameeendeshwa na wataalam wa TEHAMA Geneveva Gasper na Ramadhan Mussa kutoka Jiji la Arusha.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa