Msimamizi wa uchaguzi wa Serikali za mitaa Ndg. Msena N. Bina mapema leo tarehe 23 Septemba 2019 katika ukumbi wa mikutano wa shule ya Arusha Sekondari amekutana na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa Serikali za mitaa ngazi ya Jimbo la Arusha Mjini, Kata na mtaa kuwapatia semina elekezi juu ya uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mnamo mwezi Novemba 24, 2019.
Pamoja na kupatiwa elimu juu ya uchaguzi zoezi hili limeenda sambamba na kuapishwa kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo la Arusha Mjini, Kata na Mtaa jumla wasimamizi wasaidizi 182 wameapishwa mapema leo ambapo ngazi ya Jimbo la Arusha mijini (3), Ngazi ya Kata (25) na ngazi ya mtaa (154). Kiapo hicho kilitolewa na Hakimu mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bi. Amalia Mushi.
Katika elimu ya uchaguzi iliyotolewa na Ndg. Msena Bina alieleza kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utahusika na kuchagua wenyeviti wa mtaa pamoja na wajumbe wa kamati ya mtaa tarehe 24 Novemba 2019 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.
Uchaguzi utafanyika katika vituo vya kupigia kura katika kila mtaa na mpiga kura atatakiwa kuwa na umri wa miaka 18 au zaidi, awe raia wa Tanzania, mkazi wa mtaa husika na awe na akili timamu.
Vilevile Ndugu Msena Bina alitoa wito kwa wote wenye nia na sifa ya kugombea nafasi za uenyekiti wa Mtaa na ujumbe wa kamati ya Mtaa wajitokeze bila kusita na kuchukua fomu zitakazo kuwa zinapatikana kwenye ofisi za msimamizi msaidizi wa uchaguzi ofisi ya Kata.
Msena Bina aliongezea kwa kutaja tarehe za kuchukua fomu ya kugombea nafasi za uongozi ikiwa ni 29 Octoba kuchukua fomu na 4 Novemba 2019 kurudisha fomu hizo. Baada ya kutoa elimu hiyo kwa wasimamizi wasaidizi Msena Bina alitangaza rasmi taarifa kuwafikia wananchi kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki hivyo wakazi wote wenye sifa wajitokeze kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya Taifa.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa