Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekabidhi Sh. Bilioni 1.3 za Mikopo ya asilimia 10 robo ya kwanza ya mwaka 2021/2022 ambazo ni fedha za mapato ya ndani kwa makundi ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ambapo ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa usimamizi mzuri wa mikopo hiyo ya mapato ya ndani kwa makundi lengwa huku akisisisitiza fedha hizo zimelenga kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
Mhe. Rais Samia ameyasema hayo alipokuwa akihutubia wananchi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ikiwa ni Ziara yake ya siku mbili yenye lengo kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za Wananchi katika Mkoa huo.
Mhe. Rais Samia amesema kuwa anafurahishwa na matumizi sahihi ya fedha hizo kwa Jiji la Arusha kwani lengo la fedha hizo ni kutumika ipasavyo ili kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba ni wajibu wa viongozi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa wakati.
Aidha, Mhe Rais Samia Suhulu Hassan amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dkt. John Pima kwa utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa makundi yote lengwa yanapatiwa fedha stahiki huku akiwataka Wakurugenzi wengine wote kuiga mfano huo ili kuwawezesha wananchi hao kiuchumi.
"tunataka Wakurugenzi wengine wafanye kama Dkt. Pima, kwa hiyo Hongereni sana sana kwa mpangilio huo mzuri mliouweka" Alisema Mheshimiwa Rais Samia Suhulu Hassan.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa wataendelea kusimamia maelekezo ya Mhe Rais ya kuhakikisha kwamba mapato ya ndani ya Halmashauri yanaelekezwa kutumika kutatua kero mbalimbali za Wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. John Pima amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutoa fedha hizo kwa wananchi na kuahidi kwamba wataendelea kusimamia na kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa