Mkuu wa mkoa wa arusha mhe. Mrisho gambo ameikabidhi Halmashauri ya jiji la arusha vitambulisho 32,000 vya wafanyabiashara wadogo almaarufu kama machinga.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Tarehe 31/01/2019 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwa ni awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza Halmashauri ya Jiji la Arusha ilikabidhiwa vitambulisho 8,000 na mpaka sasa vitambulisho 6719 vimekwisha tolewa.
Pichani: Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Mhe. Gabriel Daqarro (wa kulia) akimkabidi vitambulisho vya wajasiriamali wadogo mmoja wa Maafisa Tarafa katika Jiji la Arusha Bw. Titho Cholobi.
................................................................................................................................................
Wakati wa zoezi la kukabidhi vitambulisho hivyo Mhe. Gambo ameipongeza Halmashauri kwa kulisimamia vizuri zoezi la ugawaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo na amewaagiza watumishi wanaohusika na utoaji wa vitambulisho hivyo katika ngazi ya kata kutosubiri wafanya biashara wawafate katika vituo badala yake watumie muda wao kuwafata wafanyabishara katika maeneo yao ili kurahisisha ukamilishaji wa zoezi hilo.
Kadhalika Mhe. Gambo alitolea ufafanuzi juu ya dhana nzima ya wafanyanyabishara wadogo kuwa ni miongoni mwa wale wasio katika sekta rasmi kwa maana ya kuwa hawalipi kodi ya biashara katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wala hawalipi ushuru wowote Halmashauri.
“Kitambulisho hiki kitamsaidia mjasirimali mdogo kufanya biasha zake awapo popote nchini hivyo niwaombe wafanyabiashara wadogo kujitokeza kwa wingi kuchukua vitambulisho hivi na kutoa taarifa sahihi ili kuepuka kuchukuliwa hatua kali za kisheria endapo itagundulika kuwa taarifa ni za kughushi” alisema Mhe. Gambo.
Pia amewataka Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Mhe. Gabriel Daqarro na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. Maulid Suleiman Madeni kushirikiana na watumishi katika ngazi ya kata kuzitambua nyumba au majengo katika kusaidia zoezi la ukusanyaji wa kodi ya majengo na pia Maafisa watendaji wa kata na mitaa watembelee nyumba hadi nyumba kuwafatilia walipa kodi ya majengo na wawasilishe taarifa za kila mwezi za walipa kodi katika maeneo yao.
Pichani:Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. Maulid Suleiman Madeni (wa kushoto) akimkabidi vitambulisho vya wajasiriamali wadogo Afisa Mtendaji wa kata ya Murriet iliyopo Jiji la Arusha.
.....................................................................................................................................................................
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Mhe. Gabriel Daqarro wakati akitoa taarifa yake ya zoezi la ugawaji wa vitambulisho linaloendela amesema kuwa changamoto kubwa ni wafanyabiashara kutokuwa na uelewa sahihi juu wa watu wanaostahili kupatiwa vitambulisho hivyo na pia muitikio mdogo wa wafanyabiashara kufika katika eneo la kutolea vitambulisho hivyo.
“Awali tulikabidhiwa vitambulisho 8,000 na mpaka sasa 6719 vimeshatolewa na vimebaki 1281 hivyo niwaombe watumishi katika vituo vyenu muifanye huduma hii kuwa rafiki kwa mfanyabiashara wakati tukiendelea na zoezi hilo” aliongeza Mhe. Daqarro.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa