Shule ya Msingi Maweni iliyopo kata ya Murriet Jiji la Arusha yapata fursa ya kipee katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kwa kutembelewa na wadau mbalimbali wa maendeleo ya elimu katika kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika mapema leo hii.
Shule hiyo iliyopo pembezoni mwa Jiji kwa mda mrefu tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikikumbwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji, umbali mrefu kutoka maeneo ya mjini na miundombinu mibovu ya barabara.
“Naishukuru serikali kuridhia mkataba wa kuadhimisha siku hii. Mtoto wa afrika ni namna ya kuunganisha bara letu kifikra na kusimamia ustawi wa watoto ambapo tunakumbuka mauaji ya watoto zaidi ya 500 huko Soweto mnamo mwaka 1976 ” alisema mkuu wa wilaya ya Arusha Ndg. Fabian Daqaro ambaye ndie mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Pia aliongeza kwa kusema kuwa ni jukumu la kila mtanzania kukataa vitendo vya kinyanyasaji kwa watoto na kuwapa ulinzi wa kutosha, haki ya matibabu na elimu bora kama ambavyo kauli mbiu inavyosema, maendeleo endelevu 2030, tuimarishe ulinzi na fursa kwa watoto.
Kufuatia sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 2018 amewaasa wazazi na jamii kuachana na tamaduni mbaya ya ndoa za utotoni na vitendo viovu vya ubakaji na ulawiti kwa watoto. Pia ametoa rai kwa watoto kukataa kuingizwa katika makundi mabaya na wawe watii kwa wazazi, walimu na jamii inayowazunguka.
Naye mwalimu mkuu shule ya msingi maweni Ndg. Godfrey Kishota katika risala yake ametaja uhaba wa maji kuwa ni changamoto kubwa katika shule yao na ameiomba serikali iwaboreshee miundombinu ya barabara katika shule yao kwani imekuwa kikwazo kikubwa kwa walimu na wanafunzi kuwahi shuleni hasa kipindi mvua zinaponyesha.
Katika risala ya watoto Wilaya ya Arusha , Mtoto Pendo Edward wa darasa la saba katika shule hiyo ameainisha changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na miundombinu mibovu kwa walemavu, upungufu wa walimu wenye sifa , ndoa za utotoni , vitendo vya kubakwa na kulatiwa, upungufu wa vyumba vya madarasa na pia wametaka wapewe ulinzi wa kutosha ili waweze kutimiza ndoto zao.
Miongoni mwa maonyesho yaliyoweza kuonyeshwa na wanafunzi wa kawaida na wenye matatizo ya akili (usonji) kutoka katika makampuni ya Women and Child Vision (WOCHIVI) , Connects Autism Tanzania na Compassion ni pamoja na ushonaji wa nguo, ususi wa nywele na jinsi watoto wenye usonji wanavyoweza kushiriki katika kupata elimu kupitia teknolojia ya Tehama kwa fursa sawa na wale wa kawaida
Sambamba na sherehe hizo, mgeni rasmi pia alipata fursa ya kuwatunukia vyeti na zawadi makampuni na wadau walioweza kujitoa kwa hali na mali kufanikisha siku ya Mtoto wa Afrika .
Mtoto wa Afrika ni siku ya kuwaenzi watoto zaidi ya 500waliopoteza maisha kwa kuuwawa kikatili huko mjini Soweto - South Afrika mnamo mwaka 1976
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa