Ubalozi wa China nchini Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Gold Card Foundation ya nchini China umechangia vifaa tiba katika kituo cha Afya Murriet kilichopo Jijini Arusha, vifaa hivyo ni pamoja na kitanda cha upasuaji, mashine ya usingizi na taa maalum kwa ajili ya upasuaji.
Akiongea wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika leo tarehe 19 februari, 2019 mkuu wa Mkoa wa Arusha ametoa shukurani za kwa ubalozi wa China nchini Tanzania pamoja na kampuni ya gold card kwa kuchangia vifaa hivyo vitakavyosaidia uboreshaji wa huduma ya afya katika kituo hicho.
“katika kukabiliana na changamoto ya miundombinu katika eneo hili la murriet hasa kipindi cha masika, ujenzi wa barabara ya lami unaendelea na wataalamu kutoka ofisi za Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini Tanzania (TARURA) wamehakikisha kukamilika kwake ndani ya mda mfupi ujao” alisema Rc Gambo
“Kituo hiki kwa sasa hakina gari la kubebea wagonjwa, nataka niwatoe hofu wakazi wa Murriet na kata za pembezoni kuwa gari iko njiani na mda wowote kuanzia sasa linaweza kupokelewa na kwa mujibu wa mazungumzo niliyofanya na Balozi WAN KE kutoka ubalozi wa China nchini Tanzania ameahidi kuongeza vifaa vingine vyenye thamani ya shilingi Milioni 61.5 kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma katika kituo hiki. Vifaa hivyo ni kama taa za chumba cha upasuaji, dawa za kuondolea usingizi na kitanda cha kufanyia upasuaji wagonjwa” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aidha Rc Gambo alitoa pendekezo la kuenzi jina la Mama Hadija kwa kuifanya wodi mojawapo katika kituo hicho kuwa na jina lake kwa ajili ya kumshukuru kwa moyo wake wa kizalendo na utu wake kwani kupitia yeye kutoa kiwanja chake ndipo wazo la kujenga kituo hicho cha afya likapatikana.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Mhe. Gabriel Daqarro ametolea ufafanuzi nguvu kubwa inayotumika katika kuboresha kituo hicho kuwa ni kutokana na kata hiyo kuwa pembezoni mwa mji na kuwa na idadi kubwa ya watu kutoka katika kata hiyo na kata za jirani.
“Napenda kuishukuru serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha Shilingi 700,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki kwani tangu kianze kutoa huduma kimekuwa kikipunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali za mjini”
Naye GAO WEI , Mwakilishi wa Balozi wa China nchini Tanzania amesema kuwa yeye na wawakilishi wenzie wa taasisi hiyo ni mara yao ya kwanza kufika Tanzania hivyo wamefurahia ukarimu wa Watanzania na hali ya hewa nzuri iliyopo Jijini Arusha na wataendelea kusaidia uboreshaji wa huduma za kijamii ili kuboresha mahusiano mazuri na urafiki wa nchi ya China na Tanzania.
“UDUMU URAFIKI WA CHINA NA TANZANIA”
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa