Katika kutekeleza agizo la Naibu waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii , Jinsia Wazee na watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile kukagua Makao ya kulelea watoto yatima, Halmashauri ya Jiji la Arusha imeanza kutekeleza agizo hilo jana tarehe 05/02/2017 ambapo Mganga Mkuu wa Jiji pamoja na maafisa ustawi wamekagua vituo vitano kata ya Moshono.
Wakati wa utekelezaji wa Agizo hilo lililotolewa Tarehe 29/01/2019 Jijini Dodoma katika mkutano wa mwaka wa maafisa ustawi wa jamii, baadhi Vituo vilivyopo Jijini Arusha vimekutwa na kasoro mbalimbali ikiwemo upungufu wa watumishi au walezi, kukosekana kwa maeneo ya michezo kwa watoto , ukosefu wa masanduku ya huduma ya kwanza pamoja na usiri katika taarifa za mapato na matumizi hasa katika fedha za wafadhili.
Pichani: Matukio tofautitofati yakimuonyesha Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha Dkt. Simon Chacha wakati alipokuwa katika zoezi la ukaguzi wa makao na nyumba za kulelea watoto yatima lililofanyika leo Tarehe 06/02/2019 katika baadhi ya vituo vilivopo Jijini Arusha
................................................................................................................................................................................................
Miongoni mwa kituo kilichokutwa katika hali mbaya ni kituo cha Kindness Children Center kinachomilikiwa na familia ya Bi. Christina Yohana kilichopo kata ya Kimandolu ambapo wakati wa ukaguzi uliofanywa leo Tarehe 06/2/2019 kiligundulika kutokuwa na usajili, mazingira ya ndani kutokuwa katika hali ya usafi na mrundikano wa zaidi ya watoto 40 huku huduma za malazi na chakula zikiwa za kutatanisha.
Kufuatia hali hiyo Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha Dkt. Simon Chacha aliamuru mmiliki wa kituo hicho aandikiwe barua ya kumtaka kukamilisha taratibu zote ndani ya muda mfupi huku watoto wakiandaliwa mazingira ya kupelekwa vituo vingine endapo maagizo ya serikali yatakiukwa.
Pichani: Moja ya sehemu ya malazi ya watoto katika kituo cha Kindness Children Center kinachomilikiwa na familia ya Bi. Christina Yohana kilichopo kata ya Kimandolu
...............................................................................................................................................................................
“Mpaka sasa tumeshatembelea vituo 8 kati ya vituo 28 vilivyopo Jijini hapa huku vituo 16 tu ndio vina usajili na tumegundua pia kasoro ndogondogo hivyo tumetoa maelekezo na muda wa kuyafanyia marekebisho ikiwemo pamoja na kuhakikisha vituo vinakuwa na maafisa ustawi wa jamii waliosoma kwenye vyuo vinavyotambulika na serikali ”. alisema Dkt, Chacha
“Kituo cha Neema Village Orphanage Centre ni Kizuri na kina watumishi wa kutosha kwa ajili ya kuhudumia watoto chini ya umri wa miaka miwili ukilinganisha na vituo vingine hivyo nichukue fursa hii kuwapongeza na kuwataka wamiliki wote wa makao na vituo vya kulelea watoto yatima waige mfano wa kituo hiki na wajiwekee utaratibu wa kutembeleana ilikuweza kupeana uzoefu wa mambo mbalimbali”. Aliongeza mganga mkuu huyo
Pichani: Mganga Mkuu wa Jiji na maafisa ustawi wa jamii Jiji la Arusha katika picha ya pamoja na watumishi wa kituo cha kulelea watoto cha Faraja Centre kilichopo kata ya Baraa Jjini Arusha walipotembelea kituo hicho leo Taehe 06/2/2019
....................................................................................................................................................................................................
Sambamba na zoezi hilo pia Dkt. Chacha alifanya ziara ya kushtukiza katika maabara inayojulikana na kwa jina la Victoria Labolatory Health Centre iliyopo kata ya Kimandolu na kubaini kuwa maabara hiyo haina usajili wa serikali, baadhi ya vifaa vya kupimia magonjwa havifanyi kazi, mrundikano wa takataka na uchafu usiokuwa wa lazima huku mazingira ya maabara hiyo yakiwa katika hali ya uchafu wa hali ya juu.
“Hatuwezi kufumbia macho vitendo vinavyohatarisha afya za wananchi wetu kwa kutochukua hatua dhidi ya vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya wahudumu wa afya wasiokuwa na weledi hivyo kuanzia sasa nimefungia utoaji wa huduma katika maabara hii na nichukue fursa hii kuwaomba wananchi kutohatarisha maisha yao kwa kuziamini maabara zinazoanzishwa kiholela badala yake wakatibiwe katika vituo vilivyo rasmi kwani serikali yetu imejitahidi kuboresha huduma za afya katika maeneo mengi nchini ”
Pichani: Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha Dkt. Simon Chacha akifungia maabara ya Victoria Labolatory Health Centre iliyopo kata ya Kimandolu.
....................................................................................................................................................................................
Zoezi hilo ni endelevu katika kata zote zilizopo Jijini Arusha na litaambatana na kufungia vituo ambavyo vitagundulika kutokidhi vigezo au kukikiuka kanuni na tararibu za uendeshaji wa vituo hivyo ili kulinda haki za watoto.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa