Na Mwandishi wetu.
Madiwani na Wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wamedhamiria kuhakikisha wanashirikiana kwa umoja wao kusimamia utekelezaji wa miradi kwa ufanisi na kwa wakati na hatimaye kuweza kuwaletea maendeleo zaidi wananchi wa Jiji hilo.
Hayo yamesemwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maxmillian Iranqhe mara baada ya kumalizika kwa Baraza la Madiwani la robo ya nne ya mwaka lililofanyika siku ya Alhamisi katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Mhe. Iranqhe alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ilifanikiwa kukusanya zaidi ya Shillingi billioni 17.7 ambayo ni sawa na asilimia 80 ya vyanzo vyote vya makusanyo ya ndani ambapo kiasi cha zaidi ya Shillingi billioni 9.3 ziliweza kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Jiji la Arusha zikiwa ni fedha za mapato ya ndani, Ruzuku kutoka Serikali kuu na Wafadhili mbalimbali.
Mhe. Iranqhe alisema kuwa kuelekea mwaka wa fedha 2021/2022 viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wataendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato mengi ili fedha hizo ziende kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba wamejipanga kuhakikisha utekelezaji wa miradi unafanyika kwa ufanisi na kwa wakati.
Aidha Mhe. Iranqhe amesema kwamba katika kipindi cha mwaka huu wa fedha Halmashauri inategemea kukusanya kiasi cha zaidi ya Sh. Bil. 24 kufanikisha utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za Msingi na Sekondari, matundu ya choo, ujenzi wa jengo jipya la Utawala la Halmashauri, barabara, vituo vya afya na miradi mingineyo mingi ya maendeleo.
"kwa mwaka huu fedha tunategemea kukusanya zaidi ya shilingi Bil. 24 na pesa hizo zikipatikana asilimia zaidi ya 60 zinaenda kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo Ujenzi wa jengo jipya lenye hadhi la Utawala la Halmashauri, na kwa upande wa elimu ya Msingi tumepanga kujenga madarasa 50, Elimu Sekondari madarasa 50, matundu ya choo zaidi ya 70, vyote hivi kupitia mapato yetu ya ndani" alisema Mstahiki Meya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dk. John Pima alisema kuwa kwa mwaka wa fedha uliopita wa fedha 2020/2021 moja ya maeneo ambayo Halmashauri ya Jiji la imefanya vizuri ni kwenye mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wakina mama na watu wenye ulemavu ambapo jumla ya mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 2.17 ilitolewa.
Ameongeza kwa kusema kuwa jumla ya mikopo yenye thamani Sh. Billioni 1.19 imetolewa kwa vikundi 88 vya wakina mama, mikopo yenye thamani ya Sh. Milioni 895.7 imetolewa kwa vikundi 51 kwa vijana, na walemavu mikopo yenye thamani ya Sh. million 82.8 imetolewa kwa vikundi 9.
Dk. Pima alimalizia kwa kuwapongeza wananchi kwa kuwa ni fedha walizochangia na nyingine zimerejeshwa, akiongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa mwaka huu wa fedha itaendelea kutoa mikopo hiyo huku akihimiza makundi lengwa kujitokeza kwa wingi kuchukua mikopo hiyo ili kujikwamua kiuchumi.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa