Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Jiji la Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo wakati wa kikao chake na wafanyabiashara hao mapema leo hii katika ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Katika kikao hicho Mhe. Gambo alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imejikita katika kutatua changamoto za wananchi hasa wanyonge hivyo katika harakati za kumkomboa mwananchi katika lindi la umasikini na hatimaye uchumi wa kati serikali imetengeneza vitambulisho maalum kwa ajili ya kuwatambua rasmi wafanyabiashara wadogo almaarufu kama machinga kote nchini.
Mhe. Gambo alisitiza kuwa vitambulisho hivyo ni mahsusi kwa watu wasio katika sekta rasmi wakiwemo machinga hivyo serikali haitamvumilia mfanyabiahara yoyote mwenye eneo la kufanyia biashara kutaka kuvuruga utaratibu na kuwakosesha haki wanaostahili.
“Kama lilivyo agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli vitambulisho hivyo vinawalenga wafanyabiashara ambao mzunguko wao wa mauzo ni chini ya shilingi milioni 4 kwa mwaka hivyo kigezo cha mfanyabiashara husika kupatiwa kitambuliso ni utanzania wake na si chama chake cha siasa wala dini yake”. Alisema Mhe. Gambo
“Lengo la vitambulisho hivyo si kuwatambua watu wasio katika sekta rasmi pekee bali ni pamoja na kutatua changamoto ya migogoro na migongano ya kimaslahi baina ya wwafanyabiashara wasiokuwa na maeneo rasmi na wale wenye maeneo rasmi ya kufanyia biashara zao”. Aliongeza Mhe. Gambo.
Kabla ya kuanza kikaohicho Mhe. Mrisho Gambo alitoa fursa kwa wafanyabiashara wote pamoja na uongozi wao kuainisha changamoto zao pamoja na mapendekezo yao juu ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanyia biashara ambapo Mwenyekiti wa Machinga Jiji la Arusha Bi. Amina Njoka alisema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo kama machinga ni kuhusu wafanyabiashara wenye maeneo rasmi ikiwemo madukani na masokoni kukimbia sehemu zao na kujifananisha na machinga hali inayopelekea kuonekana machinga wote ni wavunjifu wa taratibu na kanuni za nchi.
Naye mmoja wa machinga wa soko la NMC Samunge Bw. Philipo Kwaiamesema kuwa wangependa serikali ya Mkoa na Halmashauri ya Jiji iwapatie maeneo rasmi ya kufanyia biashara zao na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wafanyabiashara wa eneo la mataa ya friends corner kwani hupanga biashara zao katika eneo la barabara hivyo kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara pamoja na kuhatarisha usalama wao wenyewe.
Katika kujibu maoni na kero za wafanyabiashara hao Mhe. Gambo alisema kuwa baada ya zoezi la kutoa vitambulisho hivyo uongozi wa Jiji na Mkoa utapita katika masoko yote kukagua sehemu zilizoachwa wazi na watakabidhiwa wasiokuwa na maeneo.
Zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya vitambulisho hivyo litafanyika kwa muda wa siku tatu kuanzi Tehehe 19-21 Disemba mwaka huu katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi Ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.
MWISHO.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa