Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenister Mhagama amewataka wafanyabiashara wa Jiji la Arusha kutumia vyema kituo jumuishi cha Urasimishaji na uendelezaji wa biashara ili waweze kuongeza thamani katika biashara zao kupitia uwezeshaji na mafunzo yatakayotolewa na kituo hicho.
Waziri Mhagama ameyasema hayo Oktoba 10,2022 wakati akizindua kituo hicho akisema ifike mahali wafanyabiashara wote wawe katika mfumo wa urasimishaji ili waweze kukua kibiashara huku akiwasisitiza watendaji kuweka mpango wa kuwarasimishia wanyonge biashara zao.
Aidha Mhe. Mhagama Ameitaka MKURABITA (Mpango wa Kurasimisha Biashara za Wanyonge Tanzania) kuongeza jitihada za kuwaelimisha wafanyabiashara faida ya kurasimisha biashara pamoja na namna bora ya uendelezaji wa biashara.
Awali Waziri Mhagama alizipongeza ofisi za Mkuu wa Wilaya pamoja na Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kujenga kituo hicho kitakachosaidia uchumi wa wafanyabishara pamoja na Taifa.
Akisoma taarifa ya Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na uendelezaji wa biashara Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Hargeney Chitukuro amesema kituo hicho kilianzishwa kwa ajili ya kusaidia na kuwarasimishia wafanyabiashara kupata huduma zote za ushauri wa kibiashara pamoja na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma.
Bw. Chitukuro Alisema kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho kimeongeza ufanisi wa mapato kwa Upande Wa leseni za biashara kwa kiasi kikubwa.
"kabla kuanzishwa kituo hiki Jiji liliweza kukusanya shilingi bilioni 1.45, baada ya kituo hiki kuanza kutoa leseni za biashara Jiji limeweza kukusanya shilingi bilioni 1.65". Alisema Chitukuro.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa