MKUU wa Wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda ameagiza wafugaji wote wa mifugo wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, kuhakikisha mifugo yao, wanaweka alama za hereni za kielekroniki, ili iwasaidie kuitambua kirahisi pale inapopotea na kuisaidia Serikali kujua takwimu halisi za mifugo nchini.
Akitoa agizo hilo Oktoba 12,2022 Jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa uwekaji wa hereni hizo za kielekroniki, Mhe. Mtanda alisema hilo ni agizo la serikali ili kuitambua mifugo na mazao yake kwa njia hiyo.
Alisema lengo kubwa la Serikali kuagiza utambuzi huo, ili mifugo inapopotea ukiingia kwenye kompyuta ijulikane ilipo na kumsaidia mfugaji kupata mifugo yake kirahisi.
"Jitokezeni kuweka hereni mifugo yenu na gharama zake ndogo kwa sababu mifugo mikubwa imegharimu Sh.1750 kwa mmoja na kidogo Sh.1000"alisema.
Pia alimuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Hargeney Chitukuro na Idara ya mifugo na kilimo, kuhakikisha mifugo yote ya Jijini humo inawekewa hereni hizo.
Alisema mifugo iliyopo kwa Jiji hilo ni 16,262 ambapo katika uzinduzi huo 7000 kati ya hiyo imewekwa heleni.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Hargeney alisema katika uzinduzi huo wa utambuzi wa mifugo ng'ombe 5000 na mbuzi na kondoo 2000 wamewekewa hereni.
Alisema wafugaji watanufaika na uwekaji huo wa hereni sababu zina alama za kipekee na pale mfugaji atakapoibiwa mfugo wake, itaonekana kwenye mtandao ulipo.
"Wafugaji wote wa Jiji hili nawaomba mhakikishe mnaleta mifugo yenu kuwekwa alama hii ya kielekroniki ili iwaepushe na wizi na kuisaidia serikali kuitambua mifugo iliyopo kwa njia hii,"alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Kilimo,Ufugaji na Uvuvi, Dkt. Onesmo Mandike alisema Jiji hilo lina mifugo 16,262 kati ya hao ng'ombe 10,898,Punda 1,201 na mbuzi na kondoo 4163 ambao kati yao ng'ombe 5000 na mbuzi na kondoo 2000 imewekewa hereni.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa