Na Mwandishi wetu
WAKUU wa Sekondari katika Jiji la Arusha wamepongezwa kwa kuwezesha wanafunzi wa kidato cha Sita kufanya vizuri katika mitihani yao na kwamba hiyo ni dalili tosha kuwa Shule za Sekondari za Serikali katika Jiji hilo zinaweza kufanya vizuri na kufuta sifuri kwa wanafunzi wanaosoma katika shule zao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk.John Pima wakati akizungumza na Walimu wakuu wa Shule za Sekondari wa Jiji la Arusha katika ukumbi wa mikutano ya Jiji la Arusha.
Dk.Pima alisema kuwa anawapongeza walimu na timu nzima ilijihusisha kusimamia mitihani hatimaye kuwezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao.
Anasema kuwa pamoja na kuwa wamefanya vizuri bado wanajukumu la kuhakikisha kufanya vizuri zaidi kwa kufaulisha kwa madaraja ya juu.
“Unajua hizi shule zetu sita zinaweza kuwa katika kumi bora, inawezekana kabisa ni jitihada zinahitajika, kwani wanaufaulu wananini na sisi tunashindwa nini ?” anasema Dk.Pima
Pima alisema kuwa juhudi zaidi zinahitajika za kuhakikisha kila mwanafunzi anafanya vizuri na kuwafuatilia kwa karibu wanafunzi ambao wanadhaniwa kuwa na changamoto ikiwa ni kubaini namna yakuwasiadia waweze kufanya vizuri.
Dk. Pima aliaagiza walimu waliofanya vizuri kupatiwa zawadi ya fedha kwa kufanya vizuri na kutaka agizo hilo kutekelezwa mapema.
Afisa Elimu Sekondari Valentine Makuka akitoa ufafanuzi wa mtokeo ya kidato cha sita alisema kuwa jumla ya wanafunzi waliopata daraja la kwanza 56, Daraja la Pili wanafunzi 295 Daraja la tatu, 198 na daraja la Nne wanafunzi 8 na zero 2 ikiwa ni matokeo ya shule sita.
Bw. Makuka alisema kuwa wanafunzi hao ni kutoka shule sekondari Sita na kuwa wanafunzi waliopata daraja la mwisho walikuwa na changamoto ya kitaaluma na wengine walikuwa wagonjwa.
“Niseme kuwa baadhi ya wanafunzi walikuwa wagonjwa na wengine ni changamoto ya taaluma ila tunaahidi kufuta zero na Four kwa kuwa tunaweza .”
Makuka alisema kuwa wanauwezo wakufanya vizuri na kwamba tayari wameanza kujipanga kufikia nia njema ya kufanya vizuri kitaaluma ikiwa ni pamoja nakuingia katika kumi bora.
Naye Afisa Elimu Msingi Omary Kwesiga akizungumza na walimu hao aliwahikikishia kuwa wanauwezo wa kufanya vizuri kama ilivyo katika shule za Msingi na kwamba wanahitaji kubuni mbinu bora za kufundisha wanafunzi na kuwa karibu na wanafunzi ambao wanadhani wana changamoto katika ufaulu wao.
Pamoja na mambo mengine aliwataka kuwa na ushirikiano pamoja na malengo yakufanya vizuri kwa kufuata ufuatiliaji wa karibu ikiwa ni kuweza kubaini ni wapi wanafunzi wanakwama katika taaluma kabla yakufikia katika mitihani yao ya mwisho ya kuhitimu kidato husika.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa