Wanafunzi na wasomi wa Chuo cha Uhasibu kukabiliana na ukosefu wa ajira, waomba Serikali na wadau kuwatafutia soko la bidhaa zao.
Na Mwandishi Wetu
KATIKA kukabiliana na changamoto ya ajira Uongozi wa Chuo cha Uhasibu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wameanza kuwajengea uwezo Vijana na wasomi wa Chuo hicho wa kuanzisha shughuli za ujasirimali kwa kutumia vipaji walivyonavyo pamoja na kundeleza ubunifu waliona kwa kutumia teknolojia za kisasa na vitu vya asili.
Vijana mbali na kupata elimu ya darasani wanapata muda wa kujifunza na kuonyesha vipaji vyao pamoja na kuzalisha bidhaa bora ambazo zinawaingizia kipato.
Vijana hao wanatarajia mara baada ya kumaliza masomo yao kujiajiri na kuajiri vijana wenzao kwakuwa tayari wamepikwa na kupewa elimu sahihi ya ujasirimali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakionyesha bidhaa wanazozalisha kwa Mgeni Rasmi katika siku ya kuendeleza vipaji ambayo Mgeni rasmi ni Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk.John Pima wanasema kuwa wanajiona wenye bahati kwa kupata elimu ya kujitegemea na kuomba wadau wa maendeleo kuunga kazi zao mkono kwa kuwatafutia soko sahihi la bidhaa zao.
Rais wa Serikali ya wanafunzi Chuo cha Uhasibu Sunday Cuthbeth Masawe akishukuru kwa niaba ya wanafunzi wenzake wabunifu aliomba Serikali na wadau kuunga mkono jitihada za Vijana hao wabunifu kwa kuwatafutia masoko pamoja na kuwapatia fursa za kutoa elimu ya ugunduzi, vipaji na ubunifu lengo ikiwa ni kuibua Vijana wenye vipaji kama hivyo.
Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Gloria Kimburu akimkaribisha mgeni Rasmi kuzungumza na wanafunzi hao mara baada ya kutembelea na kuona kazi za wanafunzi wasomi wa Chuoni hapo alisema kuwa Chuo hicho kina nia njema ya kuwajengea uwezo vijana hao kwa kuendeleza vipaji vyao na hatimaye kuondokana na tatizo la Ajira pindi watakapomaliza masomo yao.
Bi Kimburu Alisema maarifa na ujuzi ni jambo muhimu sana kwa Vijana na kwamba yatawasaidia kukabiliana na dunia ya Sayansi na Teknolojia .
Pamoja na mambo mengine ameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuhamasisha elimu ya kujitegemea ikiwa na lengo la kuibua vipaji kwa vijana na kupunguza wimbi la vijana ambao hawana ajira.
Mgeni Rasmi katika siku ya ubunifu na Vipaji (Carrer Day) Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk. John Pima alisema kuwa Serikali inatambua juhudi za Vijana hao na kwamba Jiji la Arusha lina fursa lukuki za uwekezaji na kuwataka kutembelea Jiji hilo vivutio vilivyopo na kuwekeza na kwamba Vijana wanapewa kipaumbele ikiwa watakuwa tayari kuanzisha shughuli za ujasirimali wenye tija.
Dk. Pima anawakumbusha vijana kuhusu uzalendo na kupenda nchi yao na kwamba Taifa linajengwa na vijana wazalendo kuwa njia mojawapo ni kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kujipatia kipato badala ya kulalamika kuwa hakuna ajira.
Anawambia Vijana hao kuwa zipo fursa nyingi katika Jiji la Arusha kama vile mojawapo ikiwa ni fursa ya Utalii.
‘’Arusha ni kitovu cha utalii chenye vivutio leteni mawazo na kuandika mipango kazi yenu ikiwa inafaa tutawapatia ushirikiano muweze kuwekeza tuna raslimali nyinyi za uwekezaji" alisema Dk. Pima.
Pichani: Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk. John Pima alipokutana na kuzungumza na wasomi wa Chuo cha Uhasibu Jijini Arusha katika siku ya kuonesha ubunifu na vipaji vyao (Career Day) na kupata fursa ya kujionea bidhaa ambazo ni zao la vijana hao wabunifu.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa