Na Mwandishi Wetu
Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahengerwa amewataka Wanasiasa kuacha kuhujumu jitahada za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Mùngano wa Tanzania za kuleta maendeleo katika Jiji la Arusha hususani katika sekta ya Utalii.
Mhe. Mtahengerwa amesema kitendo cha wafanyabishara wadogo wadogo maarufu kama wamachinga kuandamana usiku wa kuamkia leo Aprili 29 2023, ni mbinu zinazotumiwa na Wanasiasa wenye nia ovu za kuhujumu Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kudidimiza sekta ya Utalii iliyoongezewa chachu na filamu maarufu ya "The Royal Tour".
Mhe. Mtahengerwa ametoa kauli hiyo Jijini Arusha leo tarehe 29 Aprili, 2023 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake kufuatia maandamano yaliyozua taharuki yaliyotokea hapo jana tarehe 28 Aprili, 2023 majira ya saa moja jioni katika eneo la Karakana ya Jiji la Arusha marufu Kama Depot.
Wamachinga hao walikuwa wakiandamana kwa madai mbalimbali ikiwemo kudai kuuawa kwa kijana aitwaye Izack Sangwa mkazi wa Sombetini jambo ambalo Mkuu huyo wa Wilaya amelikanusha na kueleza kuwa taarifa hizo ni za uongo na uzushi.
Mhe. Mtahengerwa ameongeza kuwa hakuna mtu yeyote aliyeuawa wala kujeruhiwa kama ilivyozushwa hapo awali bali Karakana ya Jiji ipo jirani na Kituo cha Afya Ngarenaro ambako wagonjwa wawili wajawazito walikuwa wanahamishiwa kwenda hospitali ya Rufaa ya Mount Meru na si vinginevyo.
"Wengine wameenda mbali na kusema kuna majeruhi wawili wamepigwa mpaka kuumizwa, niwaambie wale wagonjwa walikuwa hawahusiki na maandamano, walikuwa ni wajawazito na walikuwa wanaenda kupata huduma kituo cha afya Ngarenaro. Sasa inatengenezwa stori kuwa hawa watu waliumizwa na kupelekwa hospitali Mount Meru, kitu ambacho sio cha kweli ni uzushi mtupu. "aliongeza DC Mtahengerwa.
Amesema maandamano ya Wamachinga hayakuwa maandamano rasmi bali ni jambo lilikuwa limepangwa kulingana na tukio lenyewe lilivyotokea la kukamatwa kwa kijana huyo na kundi la Wamachinga kuanza kuandamana kwa wakati mmoja.
Amesema kufuatia filamu ya The Royal Tour iliyozunduliwa Jijini hapa idadi ya Watalii imeongezeka kwa kiasi kikubwa hivyo Kamati ya Usalama Wilaya ya Arusha walikubaliana kulipanga Jiji ili kuwe na sehemu ya Wamachinga ili Watalii na wageni wengine wanapokuja kutembelea Jiji la Arusha waweze kutembea vizuri bila kuwa na bugdha yoyote. Hivyo Wamachinga na Serikali walikubaliana na jambo hilo.
Mtahengerwa amesema kumekuwa na baadhi ya Wanasiasa kuwa tabia ya kuwachochea Wamachinga kurudi kwenye maeneo yao ya awali jambo ambalo amesema ni kukwamisha shughuli za kiuchumi na kurudisha nyuma jitihada zinazofanywa na viongozi jambo ambalo ni ukiukwaji wa Sheria na Taratibu.
"Kuna baadhi ya makundi ya watu unaweza kuwa mtaji wao wa kisiasa na wakaamua kufanya au kuwatumia jinsi wanavyotaka kufanikisha mahitaji yao ya kisiasa kitu ambacho kwa kweli sicho "DC Mtahengerwa
Aidha, amewataka Wanasiasa kuacha Siasa ambazo hazina tija katika Jiji la Arusha kwani Jiji hilo linatakiwa kuwa tulivu na wananchi waendelee kupata fedha na kufanya biashara katika maeneo yao waliopangiwa kwa amani na utulivu.
"Wanasiasa acheni Siasa za maji taka nawaambia kabisa hichi kinachoendelea tunakijua na malengo yake tunayajua achacheni na siasa za maji taka tujenge Arusha tulivu tuvune fedha za Watalii vinginevyo na sisi tungeamua kutumia nguvu na uwezo tulionao lakini hatutaki tuendee hivyo tunaelimishana" amesema DC Mtahengerwa.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Mtahengerwa ametoa wito kwa wafanyabiashara wote wa Jiji la Arusha kurudi kwenye maeneo yao waliopangiwa na kuacha kwenda katika maeneo yasiyo rasmi kibiashara.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa