Kundi la wasanii kutoka Mkoa wa Dar es salaam wakiongozwa na Ndg. Mbwana Himam Kipitu ambaye ni promota wa wasanii Tanzania kutoka kampuni ya “Arbaab Tv Intertainment” wamefanya ziara katika mkoa wa Arusha na kutembelea ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji Dkt. Maulid S. Madeni ikiwa ni ishara ya kutambua shughuli zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano ambapo katika ziara hiyo pia wamekutana na viongozi wa Umoja wa Vijana CCM wilaya ya Arusha.
Akizungumza katika hafla hiyo katibu wa Umoja wa Vijana CCM wilaya Ndg. Ibrahim Kijana amewashukuru na kuwakaribisha wasanii hao katika Jiji la Arusha na kuwaahidi kwamba kwa wakati mwingine watapanga muda kwaajili yakuja kuibua vipaji hivyo mchango wao katika Jamii niwamuhimu. Naye mwenyekiti wa umoja wa vijana ccm wilaya Ndg. Abubakari Saipulan amewaeleza wasanii hao kuwa wamekuja kipindi kizuri ambacho Arusha yote ni yakijani kipindi ambacho mitaa 154 ipo ndani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ushirikiano mkubwa, hamasa na miundombinu iliyopangwa kimkakati na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.
Hata hivyo mwenyekiti huyo wa vijana amewapongeza na kuwaasa wasanii hao kufikisha ujumbe kwa wananchi na kukiunga mkono chama cha Mapinduzi hususani mwenyekiti wake Dkt. John Joseph Magufuli kwa kuwafikishia wananchi yale yote mazuri yanayofanywa na serikali yao kwa njia ya sanaa hivyo sio tu kuburudisha bali kuelimisha na kuhabarisha jamii.
“Mkawasimulie huko muendako kwamba kuna mambo makubwa yamefanywa na Mhe. Rais katika Jiji hili la Arusha kwa hisani ya chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Mkuu wa wilaya Mhe. Gabriel Daqarro na Mkurugenzi wa Jiji Dkt. Maulid Madeni” aliongezea
Aidha Dkt. Madeni amewapongeza wasanii hao kwa kuwa kioo cha jamii na kuwa sehemu ya burudani lakini pia amewaasa kuufanya muziki kuwa sehemu ya ajira hivyo ni vyema Jamii ielewe na kuikuza sekta hii kwa kuiunga mkono, kuwasaidia na kuwaimarisha wasanii hivyo muziki uwe wa kimataifa ili kupunguza kundi kubwa la vijana wasio na ajira, Pia amewasisistiza wakawe chachu ya kutunza amani na usalama wa Nchi .
Sambamba na hayo Dkt. Madeni ameongeza kuwa wasanii sio tu kuburudisha bali kuna mambo mengi mazuri yanafanyika kupitia sanaa kuonyesha nini kinafanyika ndani ya Nchi na amewasihi kuendelea na moyo huo wa kuonyesha kila kitu kizuri kinachofanyika katika Nchi na kuendelea kuandika mashahiri yanayojenga na sio kuigawa Jamii au kubomoa Jamii kwa kuleta migongano baina ya viongozi kwa viongozi au serikali na wananchi. “Hivyo sanaa yenu itumieni zaidi katika kuwaunganisha watanzania na sio kuwafarakanisha ndivyo Mwenyeenzi Mungu atawapa thawabu” alisema Dkt. Madeni.
Akiiaga ofisi ya Mkurugenzi kwa niaba ya wasanii hao Ndg. Mbwana Himam Kipitu amemshukuru Mkurugenzi wa Jiji kwa mapokezi mazuri na kwamba wameguswa sana na mazungumzo hayo hivyo zawadi pekee wanayoweza kumpatia ni kumuombea dua kwa mwenyeenzi Mungu katika uongozi wake.
Mwisho.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa