Na Mwandishi Wetu
Serikali imewataka Watumishi wa Umma Jiji la Arusha kufanya kazi kwa uwajibikaji na kwa kutenda haki kwa nafasi zao wanapowahudumia wananchi ili kuwaletea maendeleo ya kweli.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deo Ndejembi (Mb) wakati wa kikao na Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji hilo.
Mhe. Ndejembi amewataka watumishi hao kutoa huduma kwa kujitoa kwa asilimia mia moja huku akisema kuwa jukumu kubwa na la msingi la watumishi hao ni kutumikia wananchi na kutoa huduma zilizotukuka.
"tunachosema, hasa ninyi mnaokaa Makao makuu ya Mikoa na Miji na Majiji hebu toeni utumishi wa Umma asilimia mia moja na kazi yenu ya msingi ni kutumikia wananchi na kazi ya serikali ni kutoa huduma iliyotukuka hivyo nanyi toeni huduma zilizotukuka" alisema Mhe. Ndejembi.
Aidha Mhe. Ndejembi amewataka watumishi hao kutenda haki kwa kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ni Serikali yenye kupenda haki na hivyo kuwaasa kutenda haki katika majukumu yao wanayoyatekeleza.
Kimsingi Mhe. Ndejembi amewasisitiza watumishi hao kuheshimu mamlaka walivyo nayo kwa kuwa mfano bora katika utekelezaji wa majukumu yao kwani kwa kufanya hivyo kutailetea Serikali taswira nzuri kwa wananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Sophia Mjema amemshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa nasaha zake kwa Watumishi hao na kusema kwamba ni muda sasa wa kuchapa kazi kwa ushirikiano na kwa weledi na hatimaye kuwaletea wananchi wa Jiji la Arusha maendeleo.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa