Katibu Tawala Wilaya ya Arusha Kamala Simba amewataka wazazi na walimu kuwa karibu na watoto wao kwa kuwashauri na kuwaelimisha dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI na Magonjwa yasiyoambukizwa.
Ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Arusha kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Felician Mtahengerwa katika maadhimisho ya kilele cha siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika katika stendi ya Kilombero.
" Kundi lilikopo kwenye hatari zaidi yakupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ni vijana katika umri balee hivyo wazazi na walimu mkae nao karibu katika kuwashauri na kuwapa elimu".
Kamala amewahamasisha wananchi wa Wilaya ya Arusha kwenda kwenye vituo takribani 24 vya afya vinavyotoa huduma ya kupima VVU ,pia wajawazito wajitokeze kwenye vituo 60 vinayotoa huduma ya Mama na Mtoto katika Wilaya ya Arusha.
Hali ya upimaji katika Wilaya ya Arusha imeshuka kutoka asilimia 3.1 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 2.3 mwaka 2022 na hali ya maambukizi kwa Mkoa wa Arusha ni asilimia 1.9, hivyo wananchi wametakiwa kutoridhishwa na hali hiyo bali waendelee kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.
Lengo la Serikali ni kutokomeza UKIMWI ikifika mwaka 2030, hivyo ili kufikia lengo hilo jamii inatakiwa kujitokeza kupima kwa wingi na watakao gundulika wanamaambukizi wanatakiwa kuanza kutumia dozi ya dawa mapema.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuviwezesha vikundi vya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kwa kuvipatia Mikopo ya Asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Arusha ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Sambamba na hilo bado juhudi za Serikali zimeendelea kuonekana kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kulipia gharama za matibabu kwa watu wanaoishi na VVU 100 sawa na kaya 20 pamoja na watu 175 wenye uraibu kwa mwaka 2022/2023.
Vilevile, katika kilele cha maadhimisho hayo Halmashauri imetoa kadi za Bima ya afya (iCHF) 210 yenye thamani za zaidi ya milioni 1 kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI sawa na kaya 35.
Pia, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na watendaji wa Vijiji kutofumbia Macho vitendo vya ukali wa kijinsia ambavyo vimeonekana ni chanzo kimoja wapo cha maambukizi ya VVU katika jamii.
Amesema, maadhimisho hayo ya siku ya UKIMWI Duniani yapo ndani ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia yaliyoanza Novemba 25 na yatahitimishwa Disemba 10,2023.
Kwa upande wake, Mratibu wa kudhibiti UKIMWI Halmashauri ya Jiji la Arusha Rosemary Tigano, amesema katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniania Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wameweza kutoa elimu kwa vijana zaidi ya 798 wa vyuo vikuu navya kati, wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari,Madereva Bodaboda, wafanyabiashara wa masoko, mafundi ujenzi, viongozi wa dini,wateja wa vilabu vya pombe za kienyeji katika kata ya Ngarenaro na Kaloleni.
Amesema jumla ya Kondom 13,791 ziligawiwa na wananchi 343 walifanyiwa uchunguzi na kati yao 194 walipimwa na 3 walibainika kuwa na maambukizi ya VVU na watu hao wameshaunganishwa na huduma za tiba na matunzo.
Maadhimisho hayo yaliambatana na utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo;Upimaji wa Sukari, Shinikizo la Damu,Uzito,Saratani ya Mlango wa Kizazi,Saratani ya tezu Dume zilizoambatana na utoaji elimu na ushauri wa Kitaalamu.
Halmashauri ya Jiji la Arusha limeadhimisha siku ya UKIMWI Duniani kwa siku 3 kuanzia Novemba 29 hadi kilele chake Disemba 1,2023 sambamba na kauli mbiu isemayo " Jamii iongeze Kutokomeza UKIMWI".
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa