Shirika lisilo la kiserikali la OIKOS limezindua mradi wa TERRA unaofadhiliwa na Taasisi ya Maendeleo na Ushirikiano ya Italy unaogharimu zaidi ya Sh. Bilioni Tatu za Kitanzania wenye lengo la kusaidia jamii za wafugaji kuboresha mbinu za uhifadhi wa chakula katika mkoa wa Arusha na kuweza kupata suluhisho la kudumu juu ya madhara yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa ambapo utaangazia hasa juu ya utunzaji wa ardhi, njia mbadala za vyanzo vya nishati, kilimo kinachozingatia majira ya nchi, kuinua kiwanda cha ngozi zitokanazo na wanyama kwa ajili ya vizazi vijavyo, kuhifadhi maeneo ya malisho ya mifungo na kuinua uelewa katika jamii.
Mradi huo uliozinduliwa leo Jana 14.09.2017 kwenye kituo cha mafunzo cha Mkuru kilichopo katika kijiji cha Uwiro ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Mrisho Mashaka Gambo ambaye ndiye mgeni rasmi, Balozi wa Italy Mh. Roberto Mengoni, wakurugenzi wa Halmashauri zote tatu zinazohusika na mradi huo ambazo ni wilaya ya Arusha, Meru na Halmashauri ya Jiji la Arusha ambapo katika miaka mitatu ijayo zitaweza kuanza kazi rasmi na kampuni ya OIKOS katika kuhakikisha kazi za mradi zinatekelezeka kikamilifu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Mrisho Gambo amesema kuwa anaunga mkono jitihada za dhati zinazofanywa na kampuni ya OIKOS katika kusaidia wakazi wa Arusha na pia ameomba miradi iendelezwe na kusimamiwa vizuri ili iweze kuwanuafaisha wakazi wa Arusha na kufikia Tanzania ya viwanda kama kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania inavyosisitiza.
“Ninayo furaha kubwa kusapoti mradi huu wa TERRA unaofadhiliwa na Taasisi ya maendeleo na ushirikiano ya Italy, hiki ni moja ya kiashiria kikuu cha ushirikiano thabiti baina Ulaya na Tanzania. Mradi huu hauhitaji pesa pekee katika kuufanikisha bali pia unahitaji umoja na mshikamano katika jamii katika kuleta mabadiliko” alisema balozi wa Italy Mh. Roberto Mengoni katika risala yake.
Aidha baada ya uzinduzi huo viongozi wote kutoka katika kampuni ya OIKOS wakiambatana na balozi wa Italy, mkuu wa mkoa, wakurugenzi na wageni wengine walipata nafasi ya kwenda kutembelea banda wanalotumia wakazi wa kijiji cha Uwiro kuhifadhia ngozi linalomilikiwa na kampuni hiyohiyo ya OIKOS chini ya mradi wa ECO-BOMA na kujionea bidhaa ghafi zinazotokana na ngozi kama ngoma na viatu vya asili sambamba na zoezi la kupanda miti lililofanywa kikamilifu na Balozi wa Italy na mkuu wa Mkoa wa Arusha kama kiashiria cha utunzaji wa mazingira.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa