Na Mwandishi Wetu
Arusha
Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranqhe amesema kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 Halmashauri ya Jiji hilo imepitisha bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni 60.6 ambapo ni ongezeko mara mbili ya bajeti waliyokuwa nayo ya shilingi bilioni 30.5 kwa mwaka wa fedha 2022/2023
Ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mapema Leo ofisini kwake Jijini Arusha na kusema kuwa Kutokana na ukuaji wa biashara na mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wa Jiji la Arusha makusanyo ya Halmashauri ya Jiji hilo yamepanda kwa asilimia miamoja kutoka bilioni 30.5 hadi shilingi bilioni 60.6.
Meya Iranqhe amebainisha kuwa ongezeko hilo la mapato limetokana na jitihada kubwa zinazofanywa na wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kushirikiana na viongozi wao.
Amesema katika bajeti hiyo ya shilingi bilioni 60.6 wameweka mikakati ya asilimia 80 ya fedha hizo kuwa zitaenda kwenye miradi ya maendeleo badala ya asilimia 70 ya hapo awali iliyokuwa ikienda kwenye miradi ya maendeleo ambapo bilioni 26.2 sawa na asilimia hamsini zikienda kwenye kundi la huduma za kiuchumi zinazo changia kuingiza mapato katika halmashauri.
Sambamba na hayo Mstahiki Meya amebainisha kuwa asilimia 50 ya bajeti hiyo ya shilingi bilioni 60.6 itaenda kwenye huduma za kijamii ikiwemo elimu na afya ili kutatua changamoto zilizopo na Watahakikisha shule zinakuwa bora na vituo vya huduma za afya zitakuwa na dawa za kutosha.
Aidha, Mstahiki meya ameeleza kuwa halmashauri hiyo itawachukulia hatua wale wote watakao bainika kucheza na mapato ya halmashauri ya Jiji hilo.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa