Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo aeleza kuridhishwa na utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa katika mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Arusha kufuatia ziara aliyoifanya awali Jijini Arusha mnamo Tarehe 23 Desemba 2019 alipotembelea mradi wa ujenzi wa wodi ya mama na mtoto mapema leo Tarehe 09 Julai 2020.Mhe. Jafo ameeleza kuwa kufuatia jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje kukamilika ujenzi wake, amefurahishwa kuona huduma zimeanza kutolewa katika jengo hilo na kutoa maelekezo kwa kaimu mhandishi wa Jiji Samweli Mshuza kuhakikisha majengo yaliyosalia nayo yanakamilika na huduma zianze kutolewa kwa wananchi kwani ndio lengo kuu la mradi huo.Mhe. Jafo ameeleza kuwa pamoja na majengo mengine ya wodi ya mama na mtoto kuendelea na ujenzi mkandarasi wa mradi huo BQ Contractors Limited asipewe nyongeza ya muda ili kukamilisha mradi kwani kipindi cha nyongeza kimekwisha hivyo mkandarasi anapaswa kukatwa malipo yake asilimia zitakazokuwa zimeainishwa kwenye mkataba wa mradi alioingia na Halmashauri ya Jiji kama ilivyo kwa mujibu wa sheria.Hospitali ya Wilaya ya Arusha ipo katika kata ya Engutoto mtaa wa Block D. Mradi wa ujenzi wa wodi ya mama na mtoto ulianza kutekelezwa Tarehe 24 Julai 2019 na kutakiwa kukamilika baada ya miezi sita. Kwa mujibu wa kaimu Mhandisi wa Jiji Bw. Samweli Mshuza changamoto za hali ya hewa zimepelekea mradi huo kutokamilika kwa muda uliokuwa umepangwa hivyo mkandarasi aliongezewa muda hadi Tarehe 31 juni 2020 japo pia hakukamilisha mradi hadi kufikia tarehe hiyo. Ujenzi wa Jengo la mama na mtoto hadi kukamilika unatarajiwa kugharimi kiasi cha fedha za kitanzania shilingi 1,395,904,605 na hivi sasa mradi umekamilika kwa asilimia 80 ambapo mkandarasi amekwishalipwa shillingi 731,950,665. Mradi huu ukikamilika unakadiriwa kutoa huduma za afya kwa kinamama takribani 200,000 na watoto zaidi ya 100,000 chini ya umri wa mika mitano.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa