Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa amezindua rasmi wiki ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatu katika ngazi ya Wilaya.
Akizungumza katika usinduzi huo Mtahengerwa amesema lengo kubwa la uzinduzi huo ni kuwapa nafasi wananchi waeleze changamoto zao kwa Serikali na Serikali ichukue jukumu la kuzitatua.
Amesema zoezi hilo ni endelevu kwani ofisi zote za Mtaa na Kata katika Jiji la Arusha zitakuwa wazi kupokea na kutatua kero za wananchi kila siku.
Aidha, Mtahengerwa amewataka wananchi kufuata utaratibu wa kupeleka malalamiko yao kwa ngazi husika kuanzia ngazi ya Mtaa, Kata na kote zikishindikana kupata majibu basi ndipo zifikishwe katika Ofisi ya Wilaya.
Vilevile, amewataka wananchi wote watakaopatiwa Mkopo wakautimie kuanzia biashara ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Kwa Upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Maxmilian Iranqe amewataka wananchi wakafanye kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo yao kupitia Mikopo watakayo patiwa.
Nae, Diwani wa Kata ya Ngarenaro ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za kijamii Isaya Doita amesema Madiwani wote watashirikiana na watendaji wa mtaa na Kata katika kuhakikisha wanasikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati katika kata zote.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Mhandisi Juma Hamsini, amesema Halmashauri iliamua kutoa fedha kiasi cha sh. Milioni 8 baada ya kupokea malalamiko ya baadhi ya wananchi wakihitaji mitaji ya biashara na fedha hizo zitagawiwa kwa wananchi hao.
Amesema, baada yakutoa fedha hizo Halmashauri itawafuatilia wananchi hao ili kuona kama fedha hizo kweli walizitumia kuanzisha biashara au laa.
Pia, Mhandisi Hamsini amesema Halmashauri imeshalipa madeni ya wazabuni kwa kiasi cha shillingi Milioni 560 huku deni lote likiwa ni Bilioni 1.5 na Halmashauri itaendelea kumaliza deni hilo.
Amesema, Halmashauri ilipata jumla ya malalamiko 12 yana wananchi walioshindwa kumudu gharama za matibabu na Halmashauri ikawachambua na kubaini wagonjwa 8 ndio wenye uhitaji na watapatiwa Bima ya afya ili waweze kumudu gharama hizo za matibabu.
Uzinduzi wa Wiki yakusikiliza Malalamiko kwa wananchi katika Wilaya ya Arusha kuliambana na utoaji viti mwendo 2 kwa wenye ulemavu,utoaji wa Mitaji takribani milioni 8, ugawaji wa kadi za Bima ya afya kwa wananchi mbalimbali na yote hayo yametokana na Wilaya kuyabaini katika usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi baada yakutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Wenezi Taifa Paulo Makonda katika ziara yake aliyoifanya Jijini Arusha.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa