Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dkt. Maulid Suleiman Madeni agundua mbinu chafu za baadhi ya wafanyabiashara wa Jiji la Arusha kujifananisha na machinga kwa kutoa bidhaa zao madukani na kwenye vibanda vya masoko na kuziweka kiholela kwa kigezo cha msamaha wa machinga kuruhusiwa kufanya biashara zao bila kubugudhiwa .
Dkt. Madeni aahidi kutokomeza kabisa hujuma hizo zifanywazo na baadhi ya wafanyabiashara wa Jiji la Arusha kwa kufanya operesheni maalum ya kuwarudisha katika maeneo yao ya awali na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wataoaidi maagizo hayo.
Katika ziara yake aliyoifanya leo Tarehe 14 /11/2018 alitembelea masoko ya Kilombero, Soko Kuu na Soko La NMC ambapo amejionea namna ambavyo baadhi ya wafanyabiashara walivyolitumia vibaya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukimbia maeneo yao rasmi na kupanga biashara zao barabarani hali inayoleta adha kubwa kwa watumiaji wa barabara na uchafuzi wa mazingira.Pichani: Baadhi ya biashara zilizowekwa katika maeneo yasiyo rasmi na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa barabara na uchafuzi wa mazingira katika Jiji la Arusha .
............................................................
“Asilimia kubwa ya wafanyabiashara wa Jiji hili hasa wenye maduka makubwa masokoni na stendi za mabasi wamekuwa wakiajiri watu wa kuwauzia biashara katika maeneo yasiyo rasmi ili waonekane kama machinga, nasema tabia hiyo iachwe mara moja kwani machinga wanafahamika na kama serikali hatutakuwa radhi kuona hadhi ya mji wetu inaharibiwa na watu wachache wasiokuwa na nia njema na Jiji letu” alisema Dkt. Madeni
“Baada ya zoezi hili la kuwarudisha wafanyabiashara katika maeneo yao ya awali nina imani kubwa mji utabaki katika hadhi yake na usafi wa hali ya juu kama ambavyo Jiji letu limekuwa likiongoza kwa sifa hiyo, hivyo niwaombe wale watakaobaki hawana maeneo ya kufanya biashara kwa maana ya machinga tutawapatia maeneo rasmi watakayoweza kuendesha shughuli zao bila tabu’’ aliongeza Mkurugenzi huyo.
............................................................
Naye Mwenyekiti wa jumuiya ya Machinga Jiji la Arusha Bi. Amina Njoka ametoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwani tangu aingie madarakani amekuwa akiwajali machinga na kuwapa vipaumbele katika kuendesha shughuli zao za kujiingizia kipato cha kila siku bila kubugudhiwa.
“Ndugu Mkurugenzi , sisi viongozi kwa niaba ya machinga wote wa Jiji la Arusha tunapenda pia tukushukuru kwa kujali wanyonge kwani tangu uteuliwe na Rais wetu umekuwa ukifatilia maslahi yetu kwa karibu na sasa upo katika harakati za kutunusuru na mihangaiko ya hapa na pale kwa kututafutia eneo rasmi litakalosaidia pia ukusanyaji wa mapato kwa maslahi ya Jiji letu na sisi tupo tayari kutoa ushirikiano kwako na viongozi wote wa Halmashauri ya Jiji letu kuhakikisha mapato yanaongezeka huku tukiuacha mji katika hali ya usafi” alimaliza kusema Mwenyekiti huyo.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa