Mkuu wa wilaya ya Arusha Ndg. Gabriel Daqaro amefanikiwa kukaa kikao cha kawaida cha kazi na maafisa tarafa, watendaji wa kata,watendaji na wenye viti wa mitaa wa halmashauri ya Jiji la Arusha kilicholenga kuzungamza nao na kujadili changamoto wanazokumbana nazo katika maeneo yao ya kazi
Miongoni mwa mambo yaliyosisitizwa ni pamoja na suala zima la ulinzi na usalama ambapo mkuu wa wilaya Ndg. Daqaro aliwaambia walengwa wa kikao hicho ambao ni maafisa tarafa, watendaji wa kata, watendaji na wenye viti wa mitaa kuwa ni jukumu lao kuhakikisha maeneo yao ya kazi yanakuwa salama wakati wote pamoja na kuripoti kwa vyombo husika na kuchukulia hatua vitendo viovu vinavyofanyika katika jamii zao vinavyoweza kuhatarisha hali ya usalama kwa mfano matukio ya ubakaji, ulawiti, matumizi ya dawa za kulevya na utekaji wa watoto.
Pia katika suala la usafi wa mazingira amesema kuwa imeonekana baadhi ya mitaa ni michafu sana hali inayopelekea uwezekano wa kutokea magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuhara na kipindupindu hivyo wahusika wakuu wanapaswa kusimamia kikamulifu kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama na safi mda wote, aidha alisisitiza kuwa katika siku za usafi kitaifa watendaji wa kata wajumueke na watumishi wenzao pamoja na wakazi katika kata husika kufanya usafi badala ya kuenda maeneo mengine.
Aidha katika suala la wananchi kupatiwa tiba kwa kadi (TIKA)mkuu wa wilaya ametoa wito kwa watendaji wa kata na mitaa kusimamia zoezi hilo kikamilifu na kushirikiana wataalamu wa masuala ya afya kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida za TIKA.
“Mradi mkubwa wa kuboresha umeme mjini unaogharimu zaidi ya million 472 unatarajiwa kuanzishwa katika halmashauri ya Jiji la Arusha mapema hivi karibuni utakaowezesha wananchi kuondokana na tatizo la kutokuwepo kwa umeme mitaani hivyo wenyeviti wa mitaa mnapaswa kuwaambia wananchi wenu kuhusu mpango huu na kutoa ushirikiano pindi wataalam wa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) pindi watakapopita katika jamii zao kutekeleza mradi huo mkubwa na wenye kuleta tija kwa jamii” Alisema mkuu wa wilaya Ndg. Gabriel Daqaro ambaye ndie mwenyekiti wa kikao hicho.
“Ni lazma watumishi wote katika katika kata kuwa na matumizi sahihi ya ofisi zao na mihuri kwani kuna baadhi ya watendaji na wenyeviti wanakosa uaminifu kwa kutumia vibaya mihuri ya serikali kujinufaisha” aliongeza mwenyekiti wa kikao.
Aidha kuhusu suala la mikutano iliyofanyika mitaani ameagiza kuwa ni lazma miuhtasari iwasilishwe katika ngazi husika na pia Katibu Tawawala Wilaya Ndg. David Mwakiposa ameagizwa kusimamia zoezi hilo kikamilifu na kutoa tarehe ya mwisho wa ukusanyaji wa miuhtasari hiyo.
Kadhalika mkuu wa wilaya Ndg. Daqaro ameeleza kuwa Kelele zinazotokana na makanisa ,bar na vilabu vya gongo ni miongoni mwa mambo ambayo yamekithiri katika baadhi ya mitaana na ni kinyume na utaratibu hivyo watendaji na wenye viti wanapaswa kudhibiti ama kuripoti katika vyombo husika kero hizo mapema iwezekanavyo.
Miongoni mwa changamoto zilizoanishwa na baadhi ya watendaji wa kata, mitaa pamoja na wenyeviti wa mitaa ni pamoja na ucheleweshwaji wa posho za vikao kutopewa ushirikiano wa kutosha na vyombo vya ulinzi na usalama pindi wanapokwenda kuripoti baadhi ya matukio yanayohatarisha hali ya usalama katika maeneo yao.
Aidha katika kikao hicho pia wataalam wa masuala ya vitambulisho vya taifa (nida) walitoa semina fupi kwa walengwa wa kikao hicho na kuwapa majukumu watendaji wote wa kata katika kusimamia zoezi la kupatiwa vitambulisho vya taifa wakazi wote kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea wanaoishi katika kata zao.
Kikao hicho kilihudhuriwa na maafisa na wataalamu mbalimbali akiwepo Katibu Tawala Wilaya ya Arusha ndg david mwakiposa,kaimu mkurugenzi wa jiji la Arusha ndg. Rebeca mongi, kaimu afisa utumishi na utawala jiji la Arusha ndg. Emmanuel mhando na kamati ya ulinzi, usalama wilaya na wataalamu wa uandikishaji wa vitambulisho vya taifa (NIDA).
MWISHO.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa