Na Mwandishi Wetu
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bw. Missaile Mussa amewataka watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha zoezi la ukusanyaji wa mapato linakuwa ajenda namba moja na kwamba wanapaswa kutambua kuwa jambo hilo ni kufa na kupona na kuwa suala hilo ni wajibu wa kila mmoja wao kwani kwa kufanya hivyo kutaleta Maendeleo ya kweli Jijini humo.
Bw. Missaile Mussa ameyasema hayo alipokuwa akiongea na Watumishi hao katika kikao kazi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha mapema Leo Jumanne Septemba 27,2022. Na kuwasisitiza kuwa lengo kama Mkoa ni kuvuka malengo zaidi ya waliyojiwekea katika ukusanyaji wa mapato.
"ninawaambia ajenda yetu kubwa ni mapato, wito wangu tukusanye mapato kwa kiwango kikubwa, sisi wote tutakuwa tukisaidiana na kumsaidia Mkurugenzi kukusanya mapato, tunataka tuvuke malengo hakuna namna" amesema Bw. Mussa.
Aidha Bw. Mussa aliongeza kwa kusema kuwa ni muhimu kwa Halmashauri hiyo kufanya vizuri katika nyanja zote na kuwasihi watumishi hao kufanya kazi kwa upendo na ushirikiano ili kuyafikia malengo waliyojiwekea.
"hatutaki alama" C", wala "B" tutakapofanyiwa tathmini, tunataka alama "A" tena alama "A+"aliongeza Bw. Missaile Mussa.
Kw upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Bw. Hargeney Chitukuro alimshukuru Katibu Tawala huyo Mkoa na kusema kwamba wameyapokea maelekezo hayo kwa ajili ya utekelezaji na kuwa hawatomwangusha na kwamba wao kama Halmashauri wapo tayari kuchapa kazi ili kuyafikia malengo.
"Tunamshukuru RAS kwa ujio wake umetutia moyo sana na ari ya kuchapa kazi, sisi kama Halmashauri tupo tayari kuyafanyia kazi maelekezo yote, tutakeleza ipasavyo na hatutoiangusha Serikali" alisema Chitukuro.
Naye Afisa Utumishi wa Jiji hilo, Bw. Gerlad Ruzika amemmshukuru RAS Mussa kwa maelekezo yake na kutoa wito kwa watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuwaletea wananchi wa Jiji la Arusha Maendeleo.
"wito wangu kwa watumishi wenzangu ni kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo kwa wananchi kwani sisi kazi yetu ni kutoa huduma stahiki kwa wananchi." alisema Bw. Ruzika.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa