Na Mwandishi wetu
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Arusha limebariki kupandishwa vyeo na madaraja kwa watumishi wanaostahili kupandishwa vyeo na madaraja ikiwa ni ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan la kutaka mamlaka husika kuhakikisha watumishi hao wanatendewa haki kwa kupandishwa vyeo na madaraja.
Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranqhe akizungumza kwa niaba ya Baraza la Madiwani alisema kuwa watumishi wanajituma katika majukumu yao na kwamba wamebariki kupandishwa kwa vyeo na madaraja.
Iranqhe alisema kuwa watumishi wakipata stahiki zao ni wazi kuwa watafanya kazi kwa bidii na kusaidia wananchi kuleta maendeleo.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk.John Pima akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Arusha alisema kuwa watumishi 33 wamepanda vyeo , zaidi ya watumishi 400 wamepandishwa madaraja na kwamba Halmashauri imetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dk. Pima aliongeza kuwa Tume ya walimu (Tanzania Teachers Commission) imeweza kuhakiki na kupandisha vyeo Walimu wapatao zaidi ya 3800 na wengine wamehamishiwa kada mbali mbali .
Mkurugenzi huyo anasema kuwa hatua ya kupandishwa vyeo kwa watumishi hao ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan Suluhu ambapo siku ya Mei Mosi 2021 aliagiza kuwa watumishi ambao wanastahili kupandishwa vyeo na madaraja kuanzia mwaka 2018 -2019 , mwaka 2019 -2020 hadi kufikia 2020 -2021 wapandishwe katika ngazi husika .
Dk. Pima alisema kuwa watumishi hao wanasubiri taratibu za kiserikali ili waweze kupata stahiki zao na kwamba Jiji la Arusha limetekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine Baraza la Madiwani limeunda kamati tatu ndogo za madiwani ambazo zitashiriki katika kufuatilia mapato, Umiliki wa kampuni za Nyama Arusha ,Ardhi na kampuni Tanzu zilizopo Jiji la Arusha.
Kamati hizo zina lengo kusaidia kuharakisha maendeleo ya Jiji la Arusha kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Wananchi walioshiriki Baraza hilo wamepongeza Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kujadili na kutoa michango katika Baraza hilo kwa ustaarabu na kwamba hatua hiyo ni kuonyesha ukomavu na nia njema yakuwaletea wananchi maendeleo.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa