"Katika robo ya kwanza kwa mwaka 2023/2024 Halmashauri ya Jiji la Arusha imeshatenga fedha kiasi cha Bilioni 3 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Yamesemwa hayo na Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Maxmilian Iranqhe alipokuwa akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani kwa robo ya kwanza mwaka 2023/2024.
Amesema fedha hizo zimepelekwa katika miradi ya afya, elimu na miundombinu ya barabara na thamani za kwenye shule mbalimbali.
Fedha hizo zimepelekwa pia kufanya maboresho kwenye dampo la takataka, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika hospitali ya Wilaya,ujenzi wa jengo la upasuaji katika hospitali ya Ngarenaro.
Alikadhalika Meya amefafanua,fedha nyingine zimepelekwa katika ununuzi wa taa za barabarani, kuna fedha za dharura kwaajili ya matengenezo ya barabara za ndani.
Amesisitiza kuwa halmashauri ipo vizuri kwasababu ya umoja na mshikamano uliopo kati ya viongozi na watendaji.
Aidha, amewataka viongozi kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ili fedha hizo ziende kwenye miradi ya maendeleo hususani kukamilisha miradi viporo.
Pia, kila mmoja akasimamie lengo la halmashauri la kukusanya mapato ya bilioni 60 kwa mwaka.
Nae, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Mhandisi Juma Hamsini amesema katika robo ya kwanza ya mwaka 2023/2024 halmashauri imeweza kukusanya mapato kwa asilimia 22.
Kikao cha baraza la madiwani kimefanyika kikiwa kimejumuisha viongozi mbalimbali wa chama cha Mapinduzi(CCM) na Serikali kwa lengo lakufanya tathimini ya utendaji wa Halmashauri.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa