Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Mhe. Gabriel Daqarro akutana na viongozi wa Dini na Madhehebu mbalimbali Jijini Arusha na kusisitiza umuhimu wa kulinda amani ikiwa ni kielelezo cha maendeleo ya wakazi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.
Akizungumza Katika mkutano huo uliofanyika jana Tarehe 28/03/2019 katika ukumbi wa Arusha School, Mhe. Daqqaro amesema kuwa viongozi wa dini wamekuwa msaada mkubwa katika malezi ya kiroho katika jamii yetu hivyo ni jukumu lao pia kusaidia kuilinda amani tuliyonayo na kutambua umuhimu wake kwa mustakabali wa Taifa hili.
“Miongoni mwa viongozi wanaosikilizwa na kuheshimika katika nchi hii ni nyie viongozi wa dini hivyo mtumie fursa hiyo kuitangaza na kuilinda amani yetu. Najua wapo wenye nia mbaya na serikali yetu , wanataka kuichafua taswira ya nchi ionekane Tanzania si mahali salama pa kuishi lakini wapuuzeni tusonge mbele” Alisema Mhe. Daqarro
“Pamoja na Taifa hili kutambua mchango wenu lakini suala la kufuata sheria na kanuni za nchi ni lazima, yapo malalamiko kwa baadhi ya nyumba za ibada kutumia vipaza sauti vikubwa kiasi cha kusababisha usumbufu katika jamii inayowazunguka. Busara itumike katika kuendesha Ibada hizo” aliongeza Mkuu wa Wilaya huyo.
Samba na hayo Mhe. Daqarro alielezea umuhimu wa viongozi hao kuhamasisha jamii kushiriki katika shuhuli na masuala kitaifa ikiwemo Mwenge wa Uhuru, kuhamasisha urasimishaji wa nyumba na makazi, upandaji wa miti, vijana kujitokeza katika mafunzo ya jeshi la akiba, vitambulisho vya wajasiriamali wadogo na pia alisisitiza umuhimu wa kufunga kamera katika nyumba za Ibada kwa ajili ya usalama sambamba na miundombinu rafiki katika nyumba hizo inayowawezesha waumini kujiokoa wakati wa dharura.
Katika mkutano huo pia wawakilishi kutoka taasisi na idara mbalimbali za serikali walipata fursa ya kutoa elimuna maelekezo mahsusi kwa viongozi hao ikiwemo mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), Taasisi ya uhifadhi wa mazingira (NEMC), Mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji (EWURA), idara ya Mipango Miji, Biashara, Ustawi wa Jamii na Usalama.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa