Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mh. Gabriel Daqarro ameviagiza vyombo vinavyoshughulikia haki na masuala ya watoto kuhakikisha matukio yote ya ukatili dhidi ya watoto yanaripotiwa katika vyombo vya dola na kesi zote zifike mahakamani ili wanaopatikana na hatia waweze kuhukumiwa.
Mhe. Daqqaro ameyasema hayo mapema leo hii wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Viwanja vya Arusha School iliyopo Jijini Arusha.
Amesema kuwa hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote wanaopatikana na hatia katika matukio ya ukatili dhidi ya watoto na kama serikali wanaendelea kupeleka maombi katika ngazi za juu ikiwezekana dhamana isiwepo katika makosa hayo ili kupunguza au kutokomeza kabisa ukatili dhidi ya watoto.
“kuna matukio mengi ya kikatili dhidi ya watoto yanafanyika katika jamii ikiwemo watoto kubakwa na kulawitiwa lakini hatua hazichukuliwi, baadhi ya wazazi na walezi hawaripoti matukio hayo na wakati mwingine kusababisha kesi zisifike mahakani hivyo niviombe vyombo vya dola kusimama kidete kuhakikisha watoto wanapata haki zao” alisema Mhe. Daqarro
“Pia nichukue fursa hii kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha mnawapa watoto ulinzi wa kutosha pamoja na kutimiza majukumu yenu ikiwemo kufuatilia maendeleo yao pamoja na kuwapa elimu kwani serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kila mwaka inatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha watoto wanapata elimu bila malipo” aliongeza Mhe. Daqarro”
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Ndg. Omary Kwesiga amesema wanafunzi wenye mahitaji maalum serikali inawajali kwa kuwatengea fedha ili waweze kujikimu katika maisha yao ya kila siku na waweze kufaulu masom yao hivyo ni wajibu wa watoto kuhakikisha wanasoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao ikiwemo kuhakikisha wanashrikishwa katika majukumu mbalimbali ili wawe viongozi bora hapo baadae.
Nao baadhi ya watoto, Ashura Juma na Issack Joseph wakati wakisoma Sera ya Watoto mbele ya mgeni rasmi walisema ni vyema sasa sheria za watoto zitiliwe mkazo ili wahalifu wasipewe dhamana kwani inaumiza kuona baadhi ya matukio yanaishia polisi bila kwenda mahakamani.
Awali maadhimisho hayo yaliambatana na maandamano kutoka makao makuu ya Jiji la Arusha hadi Arusha School pamoja na maonyesho mbalimbali ya kuibua vipaji vya watoto katika kuinua uchumi wa viwanda.
Mtoto wa Afrika ni siku ya kuwaenzi watoto zaidi ya 500 waliopoteza maisha kwa kuuwawa kikatili huko mjini Soweto - South Afrika mnamo mwaka 1976
Kauli mbiu ya mwaka huu “MTOTO NI MSINGI WA TAIFA ENDELEVU; TUMTUNZE, TUMLINDE NA KUMUENDELEZA”
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa