Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahengerwa ameitaka Halmashauri ya Jiji la Arusha kusimamia vizuri matumizi ya fedha na mapato ya Halmashauri ya Jiji hilo na kuwekeza nguvu ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Ameyasema hayo leo Februari 16,2023 Jijini Arusha Katika Mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani la robo ya pili ya Mwaka ambapo kikao hicho kiliwajumuisha Wananchi, na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Mhe. Mtahengerwa amesema kamwe hatofumbia macho matumizi mabaya ya fedha za mapato za Halmashauri ya Jiji la Arusha na pamoja na kudhibiti matumizi ya fedha na kuhakikisha wanakamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati.
Mhe. Mtahengerwa pia amelitaka Baraza hilo kufikiria vitu na miradi vikubwa ambayo itawatofautisha na majiji mengine katika upitishwaji wa bajeti na kusema kuwa Jiji la Arusha lina kila sababu ya kuhakikisha wana ongeza makisio ya bajeti kufikia bilioni 60 na kuongeza kuwa Jiji la Arusha lina vyanzo vingi vya mapato.
"tunasema Jiji la Arusha ni Jiji la kitalii, basi lazima liendane na ukubwa wa jina lake, imefika wakati Jiji la Arusha lifikirie kufanya vitu vikubwa vinanyoendana na hadhi ya jina la Jiji hili" amesema Mtahengerwa.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maximilian Matle Iranqhe amesema wamepokea maagizo hayo na wako tayari kuyafanyia kazi ili kuhakikisha wanawaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngarenaro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za jamii Jiji la Arusha Mhe. Isaya Doita wakati akiwasilisha taarifa yake katika Baraza walimshukuru Mkuu wa Wilaya na kuahidi kufanya kazi kwa Ushirikiano na Umoja kuisaidia Serikali katika kuhakikisha maendeleo yanaonekana na kuwafikia wananchi kwa kuwapatia huduma bora.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa