Na Mwandishi Wetu
Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda amewataka wazazi na walezi kutowaficha ndani watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wilayani hapo kupatiwa chanjo ya matone ya polio ili kuhakikisha usalama wa makuzi bora kwa mtoto.
Pichani : Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda akimpatia mtoto chanjo ya matone ya Polio
Mtanda ameyasema hayo katika uzinduzi wa chanjo ya matone polio katika kituo cha Afya Daraja mbili kilichopo jijini Arusha ambapo amebainisha chanjo hiyo ni salama haina madhara yoyote na inatolewa bure kwa lengo la makuzi bora ya mtoto.
"Matarajio yetu ni kuwachanja watoto wote walio chini ya miaka mitano ili kuhakikisha usalama na afya ya mtoto inaimarika na asitokee mzazi au mlezi anamzuia mtoto kupatiwa chanjo hii itakuwa ni kinyume na Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania juu ya afya njema ya mtoto,"alisema Mtanda.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Bw. Hergney Chitukuro alisema katika awamu ya kwanza takribani watoto 93,000 walichanjwa ikiwa awamu ya pili ni 1,11,808 na mwitikio huu inamaanisha elimu imeeleweka na wananchi wameelewa umuhimu wa chanjo hiyo.
"Wazazi wametuelewa kwa kufahamu umuhimu wa kuchanja watoto kwa ajili ya maisha ya watoto na hii inawasaidia wazazi kuwapunguzia adha ya matibabu mara kwa mara kutokana na mtoto kuwa na kinga ya polio,"alisema.
Hata hivyo alisisitiza wazazi kutumia kikamilifu siku nne hizo zilizotolewa na Serikali kuwapeleka katika vituo vya afya ili waweze kupata chanjo ya polio.
Nao baadhi ya wazazi na walezi wa Wilaya ya Arusha walisema chanjo hiyo ni muhimu kwa watoto wao kwani itawasaidia katika kuwakinga watoto wao wasipate ugonjwa huo wa polio.
Zoezi la utoaji chanjo ya Polio limebebwa na Kauli mbiu isemayo "kila tone la chanjo ya polio litaiweka Tanzania salama dhidi ya ugonjwa wa kupooza(Mpe Matone Okoa maisha)".
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa