Katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. Maulid Suleimani Madeni leo tarehe 31/07/2019 amekutana na viongozi wa idara ya Afya Jiji la Arusha katika ukumbi wa mikutano wa kituo cha afya Ngarenaro kuzungumzia agenda ya umuhimu wa ukusanyaji wa mapato kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.
Dkt. Madeni aliyeambatana na Mweka Hazina wa Jiji Mbwana Msangi ameonya vitendo vya baadhi ya watumishi katika vituo vya afya kutotoa stakabadhi ya mashine pindi wateja wanapokwenda kupatiwa huduma kwani inachangia kushusha mapato ya vituo husika.
Dkt. Madeni ameeleza kuwa umuhimu wa kusimamia ukusanyaji wa mapato kikamilifu unasaidia kuipunguzia mzigo serikali kuleta fedha zingine kwenye Halmashauri kama mishahara ya watumishi na fedha nyingine za miradi ya maendeleo badala yake fedha hizo zielekezwe kufufua na kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya nchi.
“Rais wetu anafanya kazi kubwa kuhakikisha miradi mikubwa ya nchi kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa umeme wa maji wa mto Rufiji (Stigler’s Gorge), ununuzi wa ndege 8 na ufufuaji wa shirika letu la ndege (ATCL) na miradi mingine mingi ya maendeleo inawezeshwa na makusanyo ya ndani . Hivyo nitoe rai kwenu wahudumu wa sekta ya afya Jiji la Arusha kusimamia kikamilifu na kwa uaminifu mkubwa ukusanyaji wa mapato” amesema Dkt. Madeni.
Katika kikao hicho pia Dkt. Madeni alipata fursa ya kusikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi ikiwa pamoja na kusisitiza kuwa idara ya afya imepewa kipaumbele kikubwa katika bajeti iliyotengwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 shilingi bilioni 3 fedha za kitanzania.
Pichani:Mweka Hazina wa Jiji Mbwana Msangiakizungumza na viongozi wa idara ya afya Jiji la Arusha
Pichani: Mganga mkuu Jiji la Arusha Simon Chacha akizungumza na viongozi wa idara ya afya Jiji la Arusha
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa