Na Mwandishi Wetu
Arusha.
Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha imejipanga kuhakikisha inachukuwa tahadhari ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Msingi Msingi Wilayani humo, Mhe. Felician Mtahengerwa akizungumza katika kikao kazi cha robo ya mwaka cha kutathimini hali ya magonjwa ya milipuko kilichofanyika leo Mei 05,2023 Kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu huyo wa Wilaya, ambapo amesema mvua hizi ni chanzo kikubwa katika kusababisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na mengineyo.
"Sisi kama viongozi na sisi kama kamati tuna wajibu na kulazimika kujadili namna gani tutaweza kukabiliana na magonjwa haya ya mlipuko hivyo ni lazima tujiweke katika tahadhari linapotokea jambo tuwe katika namna nzuri ya kukabiliana nalo."alisisitiza Mtahengerwa .
Aidha Mhe. Mtahengerwa amewaagiza Maafisa Afya wa kila kata kuwepo na maeneo ya wazi ambayo yatatumika kuwahifadhi wahanga wa magonjwa ya mlipuko endapo idadi yao itakuwa kubwa ambapo amewaomba wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo.
Ameongeza kwa kuwataka viongozi wa masoko kuweka vitakasa mikono katika maeneo yao na katika maeneo yenye misongamano ya watu wengi sambamba na kutoa elimu ya usafi wa mazingira kwa jamii.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na Katibu wa Kamati ya Afya ya Msingi, Hargeney Chitukuro amesisitiza kuwepo kwa usafishaji wa mazingira katika maeneo yenye vyombo vya kuwekea takataka.
Aidha, Chitukuro ameelekeza kusambazwa kwa barua katika Taasisi za Dini zinazoelekeza uchukuaji wa tahadhari ambapo amewataka Maafisa Afya kupiga marufuku uuzwaji wa matunda yaliyokatwa pamoja na wale wanaouza vyakula waziwazi kwa usalama wa afya za wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti Kamati ya Afya ya Msingi (PHC)B.Hindu Ali Mbwego ameiomba Mamlaka ya Maji Safi na Usafishaji wa Mazingira Jiji la Arusha(AUWSA) kuweka utaratibu wa kuyatibu maji angalau mara moja kwa wiki ili kuwakinga WATU dhidi ya magonjwa ya mlipuko hususani wanafunzi mashuleni.
Pamoja na hayo Bi.Hindu ameliomba jeshi la polisi kudhibiti na kutokomeza upikwaji na uuzwaji wa pombe za kienyeji ambazo kuchangia kwa kiasi kikubwa watu hususani vijana kupoteza maisha.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa